Habari MsetoSiasa

Ndani siku 5 kwa kutisha kumuua mbunge Florence Mutua

June 6th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAFUNZI wa Uzamili katika Chuo Kikuu cha Nairobi alifikishwa kortini Alhamisi kwa kutisha kumuua Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Busia, Bi Florence Mutua.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa mnamo Mei 27, 2019 Alex Anyolo Kikuyu alimtumia ujumbe Bi Mutua akimuonya dhidi ya kutembelea hoteli ya kifahari ya Inter-Continental ama mzunguko wa barabara inayopitia nje ya jengo la Bunge kwa vile kuna njama ya kumuua.

Bw Kikuyu alifikishwa mbele ya hakimu mwandamizi Peter Ooko ambapo alikana alimtisha Bi Mutua.

“Napinga madai kuwa nilitisha kumuua Bi Mutua. Nimechukizwa na tabia ya wanahabari kuniandama kila mahali kana kwamba nimebomoa Benki Kuu ya Kenya (CBK),” mshukiwa huyo alilalamika mahakamani.

Hakimu mwandamizi Peter Ooko. Picha/ Richard Munguti

Lakini Bw Ooko akamweleza ameruhusu wanahabri kunukuu mawasilisho kortini na kwamba “hafai kuudhika kwa vile wanahabari wanafanyakazi yao ya kujuza umma kinachoendelea.”

Kiongozi wa mashtaka Bi Susan Kurunga aliomba mahakama iamuru mshukiwa azuiliwe kwa siku saba kuwezesha polisi kukamilisha mahojiano na mashahidi na pia kuandika taarifa zao.

Akitoa uamuzi, Bw Ooko alisema inapasapasa Bw Kikuyu azuiliwe katika kituo cha Polisi cha Central Nairobi kwa muda wa siku tano kuwasaidia polisi kukamilisha uchunguzi.

“Polisi wanahitaji muda wa kutosha kukamilisha uchunguzi dhidi ya Bw Kikuyu aliyekutwa na vitambulisho vya kitaifa 13, laini 23 za simu za Safaricom na simu kadi 37,” alisema Bw Ooko.

Hakimu alisema uchunguzi utakaofanywa utawahusisha watu wengine watakaotakiwa kuhojiwa na kuandikisha taarifa kuhusu masuala haya.

Bw Ooko alisema polisi wanahitaji muda wa siku tano kuukamilisha uchunguzi.

“Utarudishwa hapa kortini Juni 14, 2019 kwa maagizo zaidi,” alisema Bw Ooko.

Mwanafunzi huyo wa somo la Uhasibu aliomba aachiliwe kwa dhamana akisema “ hawezi kutoroka kwa vile ako chuoni na anaendelea na utafiti wa taaluma ya uhasibu.”

Pia alisema mkewe ni mjamzito na anamhitaji pamoja na mtoto wao mdogo.