Ndani ya himaya ya ‘Yesu wa Tongaren’

Ndani ya himaya ya ‘Yesu wa Tongaren’

NA LEONARD ONYANGO

KIJIJI cha Lukhokwe, eneobunge la Tongaren, Kaunti ya Bungoma, huenda kikawa cha kwanza nchini na pengine kote duniani ‘kutembelewa’ na Mungu.

‘Mungu’ anatarajiwa kuzuru nyumbani kwa ‘mwanawe’ Yesu wa Tongaren kati ya Februari 24 na 26, mwaka huu 2023.

Kulingana na kiongozi wa dhehebu la New Jerusalem, Yesu wa Tongaren, wafuasi wake watatu walitumiwa ndoto (maono) zilizowafahamisha kwamba, watatembelewa na Mungu mwezi huu wa pili.

Sherehe za kumpokea Mungu zitafanyika kwa siku tatu nyumbani kwa Bw Yesu– ambaye majirani waliohojiwa na Taifa Leo walidokeza kuwa jina lake halisi ni Bw Eliud Simiyu.

Kulingana na wafuasi ambao wanafurika kanisa lake dogo, nyumbani kwa Yesu wa Tongaren kijijini Lukhokwe, ndiko Jerusalem – mji ambako Yesu Kristo katika Biblia alikulia, kufanya miujiza na kuhubiri injili.

Na kinyume cha Yesu wa Biblia, dhehebu la Yesu wa Tongaren linaendeshwa kwa ndoto au maono.

Kwa mfano, muundo au rangi ya mavazi wanayovalia wafuasi wakati wa ibada huletwa kwa njia ya ndoto. Kila muumini huota muundo na rangi ya vazi lake.

Majina wanayotumia kanisani walipewa na Mungu kupitia ndoto.

Wafuasi wa kanisa hili hutumia majina tofauti na yale yaliyo katika vitambulisho vyao vya kitaifa.

Katika kanisa hili, kila mtu anaitwa nabii au malaika.

Mwandishi wa ripoti hii alipokuwa akielekea nyumbani kwa Yesu wa Tongaren wiki hii na wenzake kutoka shirika la NTV, alipokelewa na Malaika Rachel ambaye aliwalaki katika eneo la Bondeni kwenye Barabara Kuu ya Kitale-Webuye.

Juhudi za kutaka kujua jina rasmi la Malaika Rachel alipoabiri gari lao kuelekea nyumbani kwa Yesu wa Tongaren ziligonga mwamba.

Lakini Malaika Rachel alisema alijiunga na dhehebu hilo mnamo 2014 baada ya ‘kuona’ Yesu wa Tongaren kwenye ndoto na kufikia sasa amesalia muumini mwaminifu.

“Mungu aliniletea ndoto ya Yesu (wa Tongaren) na hapo ndipo niliamini kwamba, tayari amerejea kama alivyoahidi alipokuwa akienda mbinguni,” anasema.

Waumini wa dhehebu hili wamepigwa marufuku kutumia majina yao rasmi yaliyo katika vitambulisho vya kitaifa kutokana na imani kwamba, tayari wao wamezaliwa upya baada ya kumwamini Yesu wa Tongaren.

Yesu wa Bungoma akiwa katika chumba cha kufunga katika kanisa lake kijijini Lukhokwe, Tongareni, Bungoma. PICHA | JESSE CHENGE

Malaika Rachel ndiye alitumiwa ndoto na kipaji cha kushona mavazi ya ibada.

Malaika Rachel ndiye hushona mavazi yote yanayovaliwa wakati wa ibada na waumini wa kanisa hilo.

Yeye ndiye karani wa dhehebu hilo pia hushona mavazi ya ibada yanayovaliwa na Yesu wa Tongaren.

“Mimi hushona mavazi ya ibada kwa kutumia mikono (bila kutumia cherehani). Kipaji hicho nilipewa na Mungu,” aeleza Malaika Rachel.

Rachel ndiye karani wa dhehebu hili na huandika kila kitu kinachofanyika nyumbani kwa Yesu wa Tongaren. Baadhi ya mambo anayoandika kwenye kitabu hicho cheusi ni maono ya waumini, maswali yanayoulizwa na wanahabari wanaozuru ‘Jerusalem’, majibu yanayotolewa na Yesu wa Tongaren na michango ambayo hutolewa na kila muumini dhehebu hilo linapofanya maandalizi ya sherehe.

Dhehebu hilo huandaa sherehe mara tatu kwa mwaka – Januari 1, Julai na Oktoba. Kila sherehe husherekewa kwa siku tatu ambapo kondoo, mbuzi na ng’ombe huchinjwa.

Maono na ndoto na kauli za Yesu wa Tongaren zilizonakiliwa na Malaika Rachel katika kitabu hicho cheusi, zitajumuishwa katika biblia mpya itakayoandikwa. Biblia hiyo itajulikana kama Agano Jipya Safi.

Ndani ya kanisa la Yesu wa Tongaren lina masharti makali. Wanawake hawaruhusiwi kuingia wakiwa wamevalia suruali, wamesuka nywele au kupaka rangi midomoni.

Wanaume walionyoa kando ya kichwa na kuacha nywele juu pia hawaruhusiwi kuingia katika kanisa hilo.

Waumini wanaohudhuria mazishi ni sharti wajitenge kwa siku saba kabla ya kuja kanisani.

Kulingana na Yesu wa Tongaren, watu wasiotunza Sabato (Jumamosi), wanaojipodoa, wanaovalia pete, kujichora ‘tattoo’ na kutoboa midomo au pua tayari wametiwa alama ya mnyama (shetani) nambari 666 iliyonakiliwa katika Biblia (Ufunuo 13:18).

“Watu hao ambao tayari wametiwa alama ya 666 wanaweza kuokolewa iwapo watatubu,” anasema Yesu wa Tongaren.

Dhambi nyingine ambazo Yesu wa Tongaren anasema zitazuia mabilioni ya watu kwenda mbinguni ni kula punda, ngamia, mbwa na kukosa kujitenga kwa siku saba baada ya kuhudhuria hafla za mazishi.

“Kitabu cha Hesabu 19:11 kinasema kuwa mtu anayegusa maiti ni sharti ajitenge kwa siku saba na atubu kabla ya kwenda katika hekalu la Mungu. Usipojitenga unalaaniwa. Mtu anapohudhuria mazishi inachukuliwa kuwa amegusa maiti,” anasema Yesu wa Tongaren.

Anasema ni watu 168,000 pekee watakaoenda mbinguni kote duniani. Jijini Nairobi ni watu wawili tu – ambao hawajazaliwa – watafanikiwa kwenda mbinguni, anasema Yesu wa Tongaren.

Ndani ya Kanisa, Yesu wa Tongaren huketi mbele na mkewe anayemuita Mbarikiwa au Malkia. Waumini wanaketi kimya huku wakisikiliza mahubiri ya Yesu wao. Waumini huvalia viatu vilivyotengenezwa kwa magurudumu (akala) lakini huacha viatu hivyo mlangoni wanapoingia kanisani. Yesu wa Tongaren anaingia na viatu (akala) kanisani.

Waumini wa Kanisa la Tongaren huabudu siku mbili kwa kila juma – Jumamosi na Jumapili.

“Jumamosi ndiyo Sabato ya kweli na Jumapili tunasherekea ufufuo wa huu mwili wangu,” anaeleza.

Tofauti na makanisa mengine ambayo hutilia mkazo sadaka, ni nadra kwa Yesu wa Tongaren kuzungumzia suala la sadaka au zaka.

Jumapili, ni watu saba pekee kati ya 98 – watu wazima na watoto – waliokuwa kanisani walitoa sadaka.

Yesu wa Tongaren alizaliwa mnamo 1981 kijijini Lukhokwe, eneobunge la Tongaren.

Jina lake rasmi ni Eliud Simiyu, kulingana na Mzee Mark Baraza Masinde, 52, ambaye ni jirani yake.

Bw Simuyu aliachia shule katika Kidato cha Kwanza kwenye Shule ya Upili ya Mukuyu, eneobunge la Tongaren.

Baada ya hapo akawa mkulima lakini alianza kujiita Yesu wa Tongaren mnamo 2009. Alioa akiwa na umri wa miaka 20 mnamo 2001.

Majirani waliambia Taifa Leo kuwa, kabla ya kujiita Yesu, Bw Simiyu aligongwa kichwani wakati wa mzozo wa nyumbani.

“Alikimbizwa hospitalini na alipopona alirejea nyumbani na kuanza kuhubiri huku akisema kwamba alikuwa Yesu,” akasema mmoja wa majirani.

Lakini Yesu wa Tongaren anasema alianza kupata maono ya mbinguni akiwa mtoto.

“Nilikuwa nikiona mbingu ikifunguka usiku. Wakati mwingine chumba kiling’aa kwa mwangaza hata baada ya kuzima taa. Wazazi wangu waliona mwangaza huo na wakajua kwamba, mimi sikuwa mtoto wa kawaida,” anaeleza Yesu wa Tongaren.

  • Tags

You can share this post!

Ushonaji mikeka waokoa wanawake kiuchumi Lamu

Ana kijichumba cha wafuasi kujitakasa

T L