Kimataifa

Ndege iliyombeba Makamu wa Rais yatoweka; yahofiwa imeanguka

June 10th, 2024 1 min read

NA MWANDISHI WETU

NDEGE iliyombeba Makamu wa Rais wa Malawi Saulos Chilima imeripotiwa kutoweka, huku Rais Lazarus Chakwera akiagiza shughuli za kuitafuta na uokoaji kufanywa mara moja.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Afisi ya Rais na Baraza la Mawaziri, ndege hiyo ya kijeshi ilikuwa imembeba Dkt Chilima na maafisa wengine tisa, na ilikosa kutua katika uwanja wa Mzuzu, saa nne asubuhi kama ilivyotarajiwa.

SOMA PIA: Rais wa Iran Ebrahim Raisi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni waangamia katika ajali ya helikopta

“Juhudi za maafisa wa usafiri wa anga kutafuta mawasiliano na ndege hiyo zimeambulia patupu kufikia sasa. Kwa sababu hiyo, Rais Chakwera amejulishwa kuhusu jambo hilo na ameahirisha mipango yake ya safari kwenda Bahamas na ameagiza juhudi zote zielekezwe kwenye utafutaji na uokoaji,” ikasema ripoti hiyo.

Mkasa huu unajiri wiki kadhaa tangu kuanguka kwa ndege ya helikopta iliyoua Rais Ebrahim Raisi wa Iran na maafisa wengine tisa akiwemo Waziri wa Mashauri ya Kigeni.

Inakumbusha pia mkasa wa ndege uliokumba Mkuu wa Majeshi wa Kenya Jenerali Francis Ogolla na wanajeshi wengine tisa katikati ya Aprili 2024.

SOMA PIA: Jenerali Ogolla, wanajeshi wengine 9 wafa katika ajali ya helikopta