Habari Mseto

Ndege kadha zazimwa na KCAA

November 12th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MAMLAKA ya Safari za Ndege Nchini (KCAA) imeamuru ndege saba za kampuni ya Silverstone Air zisihudumu kwa muda wa wiki moja ili kutoa nafasi kwa uchunguzi kuhusiana na msururu wa ajali ambazo zimehusisha ndege za kampuni hiyo katika siku za hivi karibuni.

Wakati huo huo, KCAA pia imesimamisha, kwa muda, leseni za kuhudumu za kampuni ya ndege ya Safe Air Company (SAC) ambayo hutoa huduma za usafirishaji wa mizigo na ile ya Adventure Aloft kwa madai ya kukiuka kanuni za usafiri wa angani.

Hayo yametangazwa Jumanne na Mkurugenzi Mkuu wa KCAA Gilbert Kibe alipofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Uchukuzi katika ukumbi wa County, jijini Nairobi.

Hata hivyo, Bw Kibe ameiambia kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Pokot Kusini David Pkosing kwamba uchunguzi unaoendeshwa na mamlaka hiyo kuhusu ajali za ndege haulengi kampuni ya Silverstone Air pekee bali kampuni zote za safari za ndege.

“Tuliamua kuanza kuchunguza Silverstone kwa sababu ndiyo ndege zake zilihusika katika ajali hivi majuzi. Nataka kuihakikishia kamati hii kuwa uchunguzi wetu unahusisha ndege zote,” akasema.

Mnamo Jumapili asubuhi ndege ya kumpuni hiyo iligonga na kuharibu ndege nyingine katika uwanja wa ndege wa Wilson, Nairobi.

Na Oktoba ndege moja ya Silverstone ililazimika kutua ghafla katika Uwanja wa Kimataifa wa Eldoret, baada ya gurudumu lake moja kupasuka dakika chache baada ya kupaa. Ndege hiyo ilikuwa safarini kutoka Lodwar ikielekea Nairobi.