Habari

Ndege mbili aina ya Boeing 737 MAX 8 zapiga abautani angani

March 12th, 2019 1 min read

CHARLES WASONGA na MASHIRIKA

NDEGE mbili aina ya Boeing 737 MAX 8 za Shirika la Ndege la Uturuki ambazo zilikuwa zikisafiri kuelekea Uingereza zililazimika kupiga abautani hewani baada ya Uingereza kuweka marufuku dhidi ya ndege hizo kusafiri katika anga yake Jumanne.

Ndege hizo zilikuwa zimeanza safari katika Uwanja wa Kimataifa wa Instanbul, Uturuki, kabla ya Mamlaka ya Kusimamia Safari za Angani nchini Uingereza kutangaza marufuku hiyo. Hii ilikuwa ni dakika chache baada ya saa saba mchana saa za Uingereza.

Na kufuatia hatua hiyo, takriban watu 300 ambao walikuwa wamepanga kusafiri kutoka Uingereza kwenda jijini Instanbul waliachwa wakihangaika katika viwanja vya ndege vya Birmingham na Gatwick.

Hatua hii imechukuliwa na Uingereza baada ya ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia Airlines ya aina hiyo kuanguka na kuwaua watu 157 mnamo Jumapili dakika sita baada ya kupaa angani.

Ndege hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka uwanja wa Kimataifa wa Bole jijini Addis Ababa kuelekea uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) Nairobi.

Zaidi ya mataifa 13 yamepiga marufuku ndege hizo zinazotengenezwa Amerika kufikia sasa. Miongoni mwao ni China, Australia, Malaysia, Singapore, India, Uingereza, Ireland, Ufaransa, Indonesia, Brazil, Afrika Kusini, Mexico, Ujerumani na Ethiopia.