Kimataifa

Ndege zaelea kwenye mafuriko na kulazimu uwanja kufungwa

April 17th, 2024 2 min read

NA MASHIRIKA

DUBAI, MILKI ZA KIARABU (UAE)

UWANJA wa ndege wa Kimataifa wa Dubai umefungwa kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa inayoendelea kushuhudiwa katika Milki za Kiarabu (UAE).

Uwanja huo wa ndege ni mojawapo ya maeneo yenye shughuli nyingi zaidi duniani.

Abiria waliokuwa wakiondoka Dubai walishauriwa kutafuta mbinu nyingine ya kusafiri.

“Tunajaribu kadri tuwezavyo kushughulikia suala hili,” wasimamizi wa uwanja huo wa ndege waliandika kwenye mtandao wao wa kijamii wa X.

Emirates ilisema abiria ambao tayari wamefika wataendelea kushughulikiwa lakini ikaonya kuwa watachukua muda mwingi sana kwenye uwanja huo wa ndege kabla ya kusafiri.

Huku mvua ikitarajiwa kuendelea kunyesha nchini humo shule na afisi za serikali pia zimefungwa na mamia kuhamia maeneo salama.

Maeneo makubwa ya nchi yamekumbwa na mvua kubwa tangu Jumapili.

Baadhi ya maeneo yalipata zaidi ya milimita 180 za mvua kati ya Jumapili na Jumanne, kulingana na Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi wa Dharura nchini.

Wastani wa mvua kwa mwaka Muscat, mji mkuu wa taifa hilo, ni kama milimita 100 – ingawa maeneo mengine ya nchi yanaweza kupata mvua zaidi ya hapo.

Kwa upande mwingine, watu 19 Oman pia wamefariki kutokana na mafuriko hayo.

Watu hao 19 ni pamoja na mtoto mchanga, kamati ya usimamizi wa dharura ilisema Jumanne, na wengine wawili hawajulikani walipo.

Kumi kati ya waliofariki walikuwa ni watoto wa shule ambao walisombwa na mafuriko wakiwa kwenye gari la shule.

Vyombo vya habari vya eneo hilo viliripoti kwamba mwanamume mzee mwenye umri wa miaka 70 pia alifariki Jumanne asubuhi gari lake liliposombwa na maji katika eneo la Ras Al Khaimah, kaskazini mwa nchi hiyo.

Huko Dubai, anga ilikuwa safi lakini katika baadhi ya maeneo barabara zilikuwa tulivu baada ya serikali kuamuru taasisi zote za serikali zifungwe.

Vyombo vya habari vya UAE na machapisho ya mitandao ya kijamii yalionyesha uharibifu mkubwa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha katika baadhi ya maeneo ya nchi, ikiwa ni pamoja na uharibifu wa miundombinu na nyumba.

Machapisho ya mitandao ya kijamii Jumanne yalionyesha barabara zilizofurika na maegesho ya magari kusombwa na maji huku serikali ikijaribu kuwaokoa waathiriwa.

Kwa upande mwingine, barabara ya Sheikh Zayed, barabara kuu nchini humo pia ilifurika na kuwafanya wengi kukwama kwenye msongamano wa magari.