Habari

Nderemo waliovuma wakishangilia matokeo

November 19th, 2019 2 min read

REGINA KINOGU NA JUMA NAMLOLA

VIFIJO na nderemo zilipamba moto Jumatatu katika kijiji cha Maragima eneobunge la Kieni, Kaunti ya Nyeri baada ya Andie Munyiri kutangazwa mwanafunzi bora kitaifa kwenye mtihani wa mwaka huu wa darasa la nane (KCPE) kwa alama 440.

Munyiri, ambaye alisomea katika shule ya Demacrest Academy iliyoko mtaa wa Uthiru, Kaunti ya Kiambu, alipata habari hizo akiwa Kaunti ya Nyeri alikokuwa ameenda kuwatembelea nyanya na babu yake.

Aliambia Taifa Leo kuwa alipata motisha ya kutia bidii masomoni baada ya babake kumwahidi angemnunulia laptopu na kumpeleka safari katika mkahawa wa The Ark ulioko Nyeri iwapo angepata alama 420 kwenda juu.

“Ahadi ya baba ilinitia motisha wa kusoma kwa bidii zaidi,” akasema mvulana huyo aliyekuwa amechangamka.

Alisema alitarajia kupata matokeo bora lakini hakuwa akidhani angeweza kuwa mwanafunzi bora wa KCPE wa mwaka wa 2019.

Alieleza kuwa matumaini yake ni kujiunga na shule ya Alliance Boys kisha chuo kikuu kusomea uhadisi ili awe kama babu yake.

Flavian Onyango kutoka shule ya wasichana ya Chakol mjini Kisumu, June Koech wa Sangalo Central iliyoko Nandi na Michael Ndung’u wa Kitengela International School katika Kaunti ya Kajiado walipata alama 439 kila mmoja katika nafasi ya pili.

Kwenye matokeo yaliyotangazwa jana na Waziri wa Elimu Profesa George Magoha, alama za juu zaidi zimepungua mwaka huu ikilinganishwa na 2018, ambapo mwanafunzi wa kwanza alikuwa na alama 453.

Waziri aliwasifu wasichana wawili walionyakua nafasi ya pili kwa kuwakilisha vyema shule za umma nchini, na kusifu matokeo hayo kuwa matunda ya uwekezaji wa serikali katika mpango wa elimu bila malipo.

“Wanafunzi katika shule za umma wamepata matokeo bora sawa na wenzao katika shule za kibinafsi. Hili ni dhihirisho kuwa mpango wa Elimu Bila Malipo umefana na walimu wetu wamejitolea, hata baada ya kulemewa na idadi kubwa ya wanafunzi. Pia inaonyesha kuwa wasichana wetu wanakabiliana vilivyo na wavulana katika masomo,” akasema.

Mbali na alama ya juu kushuka, wanafunzi waliopata alama 400 na zaidi pia walipungua kutoka 12,273 mwaka jana hadi 9,770 mwaka huu.

“Lakini watahiniwa waliopata alama kati ya 301 na 400 waliongezeka kutoka 223,862 mwaka jana hadi 243,320 mwaka huu,” akasema Prof Magoha.

Sawa na mwaka uliopita, wasichana waling’ara kwenye masomo ya Kiingereza, Kiswahili na Lugha ya Ishara huku wavulana wakiwa bora katika Hesabu, Sayansi na Elimu Jamii na Dini.

Waliopata alama kati ya 201 na 300 walipungua kutoka 576,346 hadi 566,886. Lakini waliopata kati ya alama 101 na 200 waliongezeka kutoka 235,555 mwaka 2018 hadi 262,307 huku waliopata kati ya 0 na 100 wakipungua kutoka 2,198 hadi 1,173 pekee mwaka huu.

Waziri alisema mwaka huu wanafunzi walemavu walikuwa 2,407 na wa kwanza alipata alama 414.

“Pia watahiniwa 211 walio na mahitaji maalumu walipata kati ya alama 300 na 400. Nataka nisisitize kuwa serikali imejitolea kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalum wanapata elimu sawa na wenzao. Tunapanga kuanzisha kituo maalum Nairobi kitakachokuwa na vifaa vya kisasa vya kuwawezesha kujifunza ujuzi mbalimbali,” akasema.

Kuhusu udanganyifu, waziri alisema ni wanafunzi wanne pekee waliopatikana wakijaribu kuhusisha watu wengine kuwafanyia mtihani. Hatua zilichukuliwa na kuwaondoa kutoka kwa mtihani huo.

Upungufu huo wa wanafunzi waliojihusisha na udanganyifu ni ushindi mkubwa kwa serikali, ikizingatiwa kuwa miaka ya nyuma watahiniwa wasiopungua 1,000 wamekuwa wakihusika kila mwaka.

Sawa na mwaka jana ambapo aliyekuwa waziri wa Elimu Bi Amina Mohamed alisema watahiniwa wote wangejiunga na shule za upili, Prof Magoha alisema hakuna mwanafunzi atakayeachwa nyumbani.

Kilichosadifu jana ni jinsi ambavyo matokeo hayo yalitangazwa siku moja nyuma ya ilivyokuwa mwaka jana, ambapo Waziri Amina aliyatangaza akiwa mjini Mombasa, Novemba 19.