Habari Mseto

Ndevu hizi anazofuga kuiga Nabii Mohamed zimemtia mashakani kila mara

May 24th, 2018 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

MWANAHARAKATI wa kutetea haki za kijamii katika kaunti ya Lamu amelalamikia mateso anayokumbana nayo mikononi mwa walinda usalama hasa wale walioko nje ya Lamu kutokana na ndevu zake ndefu.

Bw Ahmed Famau,32, anasema ndevu zake sasa zimegeuka kuwa kisirani katika maisha yake kwani maafisa wa usalama wamekuwa wakimkamata kwa kumdhania kuwa mshirika wa kundi la kigaidi la Al-Shabaab.

Katika mahojiano ya kipekee na Taifa Leo mjini Lamu, Bw Famau alisema amekamatwa zaidi ya mara nne katika kipindi cha miaka minne iliyopita kwa kuhusishwa na Al-Shabaab eti kwa sababu ya kufuga ndevu ndefu.

Anasema mara ya kwanza kukamatwa ilikuwa 2015 wakati amri ya kutotoka nje usiku almaarufu kafyu ilipokuwa ikiendelezwa Lamu.

Anasema pia amewahi kukamatwa katika uwanja wa ndege kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) jijini Nairobi ambapo alizuiliwa kwa siku tatu kwa sababu ya ndevu zake ndefu.

Anasema ndevu zake pia zimemfanya kukamatwa na polisi mjini Mombasa na kuzuiliwa kwa wiki nzima.

Pia amewahi kukamatwa na kuzuiliwa na polisi katika uwanja wa ndege akiwa amesafiri kurudi Kenya kutoka ng’ambo.

Ahmed Famau amekamatwa mara nne na polisi kwa kudhaniwa kuwa mwanachama wa Al-Shabaab. Picha/ Kalume Kazungu

Bw Famau ambaye pia ni mshauri wa vijana hasa kuhusiana na masuala ya kujiepusha na itikadi kali na ugaidi eneo hilo alisema ufugaji wake wa ndevu unatokana na kuiga tabia za Mtume Mohamed (S.A.W) ambaye pia alifuga ndevu wakati wa enzi yake.

“Mimi sina tatizo na maafisa wa usalama hapa Lamu lakini kila mara ninaposafiri nje ya Lamu, mimi hupata shida kutokana na ndevu zangu ndefu. Tunapofika kwenye vizuizi vya polisi kukaguliwa pamoja na wasafiri wenzangu, mimi huwekwa kando kwanza.

Aghalabu utampata polisi akibadili bunduki yake kutoka upande wa nyuma na kuiweka mbele hasa anaponitazama. Mimi si Al-Shabaab. Ndevu zangu nimezifuga  hadi kuwa ndefu hivi ili kumuiga Nabii Mohamed (S.A.W).

Walinda usalama waache kutuhangaisha baadhi yetu ambao tunafuga ndevu. Tunafuga hizi ndevu kwa nia njema,” akasema Bw Famau.

Aidha amewataka vijana kote Lamu na Kenya kwa jumla kujiepusha na ugaidi na badala yake kushirikiana na serikali hasa vyombo vya usalama katika kuhakikisha amani na utulivu unadumishwa kote nchini.

“Licha ya yote ninayokumbana nayo, mimi ni rafiki wa maafisa wa usalama hasa Lamu. Ninaipenda sana nchi yangu na hii ndiyo sababu nitaendelea kuwasihi vijana wenzangu kushirikiana na vyombo vya usalama ili kuhakikisha amani inadumishwa Kenya,” akasema Bw Famau.