Siasa

Ndindi Nyoro atakubali wito wa kushirikiana na Maina Njenga?

January 18th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

HATUA ya aliyekua kiongozi wa kundi la Mungiki, Bw Maina Njenga, kumrai mbunge Ndindi Nyoro (Kiharu) kubuni muungano wa kisiasa, imeibua maswali kuhusu ikiwa mkakati huo ndiyo njia mpya ya wawili hao kumpindua Naibu Rais Rigathi Gachagua kama kiongozi wa kisiasa wa Mlima Kenya.

Mnamo Jumatano, Bw Njenga alisema yuko tayari “kushirikiana na Bw Nyoro kulikomboa eneo la Mlima Kenya kwa kuleta usawa kwenye uongozi wake.”

Bw Maina alitoa kauli hiyo kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio, akisema kwamba “wakati umefika sauti ya kisiasa ya eneo hilo ianze kusikika tena.”

Akionekana kumsifia Bw Nyoro kwa juhudi ambazo amekuwa akiendesha kuboresha nafasi yake kuchukua uongozi wa ukanda huo, Bw Maina alisema yuko tayari kuungana na mbunge huyo na wabunge wenzake wanaomuunga mkono “ili kuwakomboa wenyeji”.

“Ikiwa leo ninaweza kukutana na Bw Nyoro, ninaweza kumnunulia chai,” akasema Bw Njenga.

Aliyekuwa kiongozi wa Mungiki Bw Maina Njenga ahutubia wanahabari nyumbani kwake Ongata Rongai katika Kaunti ya Kajiado mnamo Januari 1, 2024. PICHA | EVANS HABIL

Kwenye mahojiano hayo, Bw Njenga aliunga mkono malalamishi yaliyotolewa majuzi na viongozi kutoka Kaunti ya Murang’a, kwamba kaunti hiyo haijawahi kumtoa Rais au Naibu Rais katika eneo la Kati, hivyo wakati wake kufanya hivyo umefika.

Viongozi hao waliongozwa na Seneta Joe Nyutu (Murang’a), wakisema kuwa lengo kuu la kushinikiza Bw Nyoro kuteuliwa kama mgombea-mwenza na Rais William Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa 2027 ni angaa “kuhakikisha Kaunti ya Murang’a imeonja uongozi wa kitaifa”.

“Tunamrai Dkt Ruto kumteua Bw Nyoro kama mgombea-mwenza wake 2027 kwani baada ya kuzungumza na watu wetu, tumebaini kwamba yeye ndiye kiongozi maarufu zaidi kwa sasa,” akasema Bw Nyutu.

Kulingana na wadasisi wa siasa, mielekeo hiyo miwili ni tishio kubwa la kisiasa kwa Bw Gachagua, kwani msukumo wa viongozi hao ni kutoridhishwa na uongozi wa Bw Gachagua.

“Kujitokeza waziwazi kwa viongozi hao wawili kunafaa kumweka tumbojoto kisiasa Bw Gachagua, kwani wawili hao ni watu wanaoendelea kujizolea umaarufu na ushawishi fulani kisiasa. Bw Njenga ana umaarufu mkubwa miongoni mwa vijana huku Bw Nyoro akiibukia pia kuwa maarufu miongoni mwa vijana. Rekodi nzuri ya maendeleo katika eneobunge lake la kiharu pia imeinua nyota yake kisiasa nchini,” asema Bw Mark Bichachi, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Anasema kuwa hata ikiwa viongozi hao wawili wako katika mirengo miwili tofauti ya kisiasa-Azimio na Kenya Kwanza-wote wameunganishwa na lengo moja: kubuni sauti na mwelekeo mpya wa kisiasa wa Mlima Kenya.

“Bila shaka, licha ya viongozi hao wawili kuwa katika mirengo tofauti ya kisiasa, wanaunganishwa pamoja na lengo lao la kubuni mwelekeo mpya Mlimani. Ni hali inayofaa tumbojoto Bw Gachagua kuhusu mustakabali wake kisiasa,” akasema Bw Bichachi.