Habari Mseto

Ndingi kutengewa siku maalum kukumbukwa corona ikidhibitiwa

April 8th, 2020 1 min read

Na WANDERI KAMAU

SERIKALI itatenga siku maalum kumkumbuka Askofu Ndingi Mwana a’Nzeki wa Kanisa Katoliki baada ya virusi vya corona kukabiliwa.

Kwenye ujumbe wake wakati wa mazishi ya askofu huyo, Rais Uhuru Kenyatta alisema Wakenya watachukua nafasi hiyo kumwomboleza kutokana na mchango mkubwa aliotekeleza katika maendeleo na demokrasia nchini.

Askofu Ndingi, ambaye alifariki Jumanne wiki iliyopita akiwa na umri wa miaka 89 alizikwa jana kwenye ibada iliyohudhuriwa na waombolezaji takriban 100.

“Tutatenga siku maalum baada ya janga la virusi vya corona kupungua ili kusherehekea mchango aliofanya katika maisha yake. Yalikuwa mapenzi ya Wakenya wengi kujumuika pamoja kumuaga, lakini haingewezekana kutokana na tisho la virusi hivyo,” akasema Rais Kenyatta.

Rais alitarajiwa kuwahutubia waliohudhuria kwa njia ya video kutoka Ikulu, lakini akamtuma mwakilishi baada ya hitilafu za kimitambo kutokea.

Hafla hiyo ya kumuaga Askofu Ndingi iliongozwa na Kadinali John Njue, ambaye pia ndiye Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Nairobi.

Waliohudhuria walikaa kwa umbali wa mita moja, ikiwa mojawapo ya maagizo ambayo yametolewa na serikali kuhusu njia za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Kadinali Njue alimtaja marehemu kama kiongozi aliyesimama kidete kutetea nafasi ya kanisa na demokrasia nchini, hasa wakati ilikuwa vigumu kwa viongozi wa kidini kufanya hivyo.

Mwili wa marehemu uliwekwa katika eneo maalum ambapo maaskofu waliohudumu katika dayosisi ya Nairobi huwa wanawekwa wanapofariki.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria hafla hiyo ni kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, Jaji Mkuu David Maraga, Maspika Justin Muturi (Bunge la Kitaifa) na Kenneth Lusaka (Seneti).

Marehemu alizaliwa mnamo Desemba 25, 1930 katika eneo la Mwala, Kaunti ya Machakos. Alitawazwa rasmi kama kasisi mnamo 1961.

Alihudumu katika dayosisi ya Machakos (1969-1971) na askofu wa Dayosisi ya Nakuru (1972-1996).

Baadaye, alihudumu kama askofu wa Dayosisi ya Nairobi kutoka 1997 hadi alipostaafu mnamo 2007.