Ndiritu Muriithi aisuta IEBC kwa kuwafungia nje ya Bomas

Ndiritu Muriithi aisuta IEBC kwa kuwafungia nje ya Bomas

NA ELISHAPHAN WACHIRA

MWENYEKITI wa kampeni za mrengo wa Azimio-One Kenya Alliance Ndiritu Muriithi, amemsuta mwenyekiti wa IEBC kwa kile anachodai ni ukandamizaji wa haki.

Akizungumza nje ya lango la kituo cha kujumlisha kura cha Bomas, Muriithi alisema kwamba haikuhalisi IEBC kuwazuia mawakala wa wagombeaji kama yeye kuingia kwenye kituo hicho.

“Kulikuwa na haja gani kutupea cheti hiki kuonyesha sisi tu mawakala wa Wagombeaji ilhali hawaturuhusu kuingia ndani,” alisema Muriithi.

Muriithi alisema kwamba tume ya IEBC itakuwa ya kulaumiwa, iwapo jambo lolote lingetokea kuanzia Jumapili jioni.

“IEBC lazima iwe tayari kujibu lolote litakalotokea kuanzia sasa. Yafaa IEBC iwaambie Maafisa wake kutowazuilia mawakala wa Wagombea kuingia ndani kwa kuwa wana kibali,” aliongezea Muriithi.

IEBC hapo jana Jumapili ilitoa masharti mapya kuzuia watu wengi kusongamana kituoni humo, ikisema kwamba hatua hiyo ingeharakisha shughuli nzima ya ujumlishaji wa kura. Ni hatua ambayo haikupokelewa kwa mbwembwe na vigogo wa mrengo wa Azimio la Umoja, ambao walidai kwamba IEBC ilikuwa na njama fiche.

Tayari kituo hicho cha kujumlisha kura kina idadi kubwa ya maafisa wa kupambana na ghasia, ndani na nje ya lango lake, ili kumzuia yeyote aliye na wazo la kuzua rabsha kituoni humo.

Kati ya viongozi waliotambulika kuzuiliwa kwenye lango la kituo hicho cha Bomas ni Gavana anayeondoka wa Laikipia Ndiritu Muriithi, Gavana mteule wa Kisumu Profesa Anyang Nyong’o, mbunge wa zamani Fred Gumo kati ya wengine.

  • Tags

You can share this post!

Nani kama Wakenya!

ODM matumaini tele kuhifadhi ugavana Mombasa

T L