Makala

NDIVYO SIVYO: Baadhi ya tafsiri za ilani katika matatu simango kwa Kiswahili

October 2nd, 2019 2 min read

Na ENOCK NYARIKI

KATIKA makala yetu tutaona jinsi dhana kuwa Kiswahili ni lugha ngumu inavyotumiwa kama udhuru wa kuziboronga tafsiri za kauli au maneno ya msingi kabisa yanayolenga hadhira pana ya wasomaji.

Katika mojawapo ya mabasi ambayo huwasafirisha abiria kwenye barabara ya Nairobi-Ngong-Kiserian, mlibandikwa ilani ifuatayo kwa lugha ya Kiingereza kisha chini yake ikatafsiriwa kwa Kiswahili:

Beware of pick-pocketers,

The sacco will not bear responsibility.

Chunga wezi wa kuingiza mikono kwa mifuko na mikoba,

Shirika *halitagaramikia chochote.

By management, NANGKIS Sacco.

Lililoyavuta makini yangu kwenye ilani hiyo ni tafsiri ya Kiswahili ya ujumbe huo ulioandikwa kwa Kiingereza – ingawa hakika nikidhani kuwa ‘pick-pocketers’ si neno la Kiingereza jinsi lisivyo neno jingine ‘guider’.

Hata hivyo, katika siku zangu za uanafunzi katika shule ya upili niliwasikia wengi wakisema kwa Kiingereza kibaya kwamba ‘God is our guider’.

Nimewahi kukumbana na neno ‘pickpocket’ ila sijui kama lipo ‘pickpockecters’.

Iwapo lipo, basi ninaomba udhuru. Lengo langu hata hivyo si ‘kukichokonoa’ Kiingereza maadamu kina wenyewe.

Tafsiri iliyofanywa na utawala (Ushirika wa wenye Matatu) wa barabara ya Nairobi- Ngong-Kiserian (NANGKIS) ilikuwa na makosa tumbi nzima ila nitayaangazia machache tu.

Kwanza, neno la Kiingereza ‘beware’, katika muktadha huo haliwezi abadani kuwa na tafsiri ya chunga. Neno chunga lina zaidi ya maana sita ingawa hakuna moja kati ya maana hizo inayolikumbatia neno ‘beware’ au ‘be wary’ ama ‘be cautious’. Kamusi ya Karne ya 21 inatoa fasili za neno chunga ifuatavyo:

Kwanza, ni kuwapeleka wanyama malishoni na kuwalinda wasiibwe.

Pili, ni kulinda. Tatu, ni kudhibiti. Nne, ni kusimamia. Tano, ni kuwaongoza waumini wa Kikristo na sita, ni kuchuja unga kutoka kwenye mchanganyiko wa unga na chenga.

Kwa hiyo, fasiri faafu ya neno ‘beware’ ingalikuwa tahadhari au tazama; ingawa huenda neno “tazama” lisiibue uzito unaokusudiwa hapa. Kifungu ‘beware of pickpockets’ kingalikuwa: Tahadhari dhidi ya sinzia au vibaka.

Nimeitafsiri dhana ‘of’ kuwa ‘dhidi’ kwa sababu katika muktadha ambamo imetumiwa inaibua dhana nyingine inayokaribiana sana nayo ambayo ni ‘against’.

Waama mtu hutahadharishwa dhidi ya jambo na kushauriwa kuhusu jingine.

Basi isingekuwa mwafaka kwetu kusema ‘tahadhari kuhusu sinzia au vibaka’.

Hata hivyo, tunaposema “chunga wezi wa kuingiza mikono kwa mifuko na mikoba”, tafsiri hiyo haina tofauti sana na ile iliyozoelewa sana na wanafunzi wa shule ya chekechea: “…huyu ameingia kwenye mkoba wangu.”

(ITAENDELEA)