Makala

NDIVYO SIVYO: Hakuna neno ‘thamana’ katika lugha ya Kiswahili

July 17th, 2019 2 min read

Na ENOCK NYARIKI

BAADHI ya watu huyatumia maneno “thamana” au “dhamana” kwa maana ya kitu kinachothaminiwa au kuchukuliwa kuwa bora kutokana na umuhimu wake katika jamii.

Nisingelitumia neno jingine faafu kutolea fasili maana hiyo ambayo hudhaniwa kuwasilishwa na maneno hayo mawili ila kitenzi ‘kinachothaminiwa’ .

Hata hivyo, ningependa kusisitiza kwamba Kiswahili hakina neno “thamana”. Halipo hasha!

Lipo neno dhamana ingawa lina maana tofauti kabisa na hiyo ambayo baadhi ya watu hulitumia kwayo.

Hakika, neno hilo lina maana moja ambayo imeenea sana katika uwanja wa sheria.

Hutumiwa kurejelea mali au pesa zinazotolewa mahakamani ili mshtakiwa aachiliwe huru kwa muda fulani kesi yake inapoendelea kusikilizwa. Kwa njia nyingine, dhamana humwepushia mshtakiwa udhia wa kuzuiliwa kwenye seli.

Hapa nimelitumia neno seli badala ya ‘korokoroni’ au ‘rumande’ kwa sababu maneno hayo mawili yana utata ambao nitauzungumzia katika makala tofauti.

Kamusi ya Karne ya 21 inaeleza kuwa maana ya pili ya dhamana ni wadhifa au mamlaka ila hakika maana hii haijitokezi sana katika mazungumzo ya kila siku.

Dhamana ni nomino ambayo imeundwa kutokana na kitenzi dhamini.

Ifahamike hata hivyo kwamba, kitenzi hicho kina maana nyingine ambazo hazipati fasili yazo katika nomino dhamana. Yaani, si ‘dhamini’ zote ambazo zinaweza kutumiwa kuunda nomino dhamana.

Asiye na uwezo

Mathalani, maana nyingine ya neno dhamini ni kumpa fedha mtu asiye na uwezo ili kutatua shida fulani kwa mfano elimu au matibabu.

Mfano: Kaka yake ndiye anayemdhamini masomoni.

Hapa, hatuwezi kusema kwamba kaka yake ndiye anayemtolea “dhamana” masomoni kwa maana hiyo hiyo.

Neno thamani nalo lina maana ya ubora wa kitu kutokana na umuhimu wake katika jamii. Kwa mfano, kwa baadhi ya watu, magari na majumba ya kifahari ni vitu vyenye thamani kwao.

Tunaweza kusema kwa yakini kuwa neno thamani lina ukuruba na kitenzi thamini. Mathalani, iwapo magari na majumba ni vitu vyenye thamani kwa watu hao, basi wanavithamini.

Kiswahili kina neno dhamani ila nalo hutumiwa kwa nadra sana kurejelea mwisho wa msimu wa upepo uvumao kutoka Kusini kuelekea Afrika Mashariki.

Neno hilo halipaswi kutumiwa kurejelea ubora wa kitu kutokana na umuhimu wake katika jamii!

Kitenzi thamini ambacho watu hukitamka kama “dhamini” kutokana na kasoro katika ala ya kutamkia sauti {dh} na {th}, kina maana mbili. Kwanza ni kadiria ubora na bei ya kitu.

Pili ni kustahi, kupenda, kuheshimu, kutia maanani n.k. Mfano: Asiyekujua hakuthamini.