Makala

NDIVYO SIVYO: Idadi nne za asili ya kigeni hazichukui viambishi vyovyote katika matumizi

March 8th, 2018 2 min read

Na ENOCK NYARIKI

Viambishi awali huwakilisha dhana mbalimbali katika lugha ya Kiswahili. Dhana hizo ni pamoja na nafsi, ngeli na umoja au wingi. Hakika, dhana ya nafsi na umoja au wingi zinaweza kujitokeza chini ya ngeli ila tumezigawa hivyo ili kurahisisha maelezo yetu.

Viwakilishi nafsi ni maneno kamili au viambishi vinavyosimamia nomino za viumbe vyenye uhai. Kwa upande mwingine, viambishi vya idadi husaidia katika kubainisha iwapo sentensi inayohusika iko katika hali ya umoja au wingi.

Ni rahisi sana kuhesabu nambari au takwimu katika lugha ya Kiingereza kuliko ilivyo katika lugha ya Kiswahili. Jambo hilo hutokea hivyo kwa sababu lugha ya Kiingereza haina upatanisho wa kisarufi ambao ni lazima uzingatiwe wakati wa kuzitaja idadi.

Kosa la kuhesabu nambari hujitokeza sana katika idadi za msingi. Hizi ambazo tumezirejelea hapa kama idadi za msingi ni kuanzia moja hadi kumi.

Kosa linalotokea wakati wa kuhesabu nambari limerithiwa kutoka mfumo wa zamani wa uainishaji wa maneno katika ngeli ambapo mkazo ulitiwa katika viambishi vya nomino wala si aina nyingine za maneno.

Baadhi ya wanafunzi walioupitia mfumo huo hawafahamu wakati wa kuviongeza viambishi katika idadi fulani na wakati wa kuviacha nje viambishi hivyo.

Matokeo yake ni kufanyika kwa makosa yafuatayo:
*Wanafunzi kumi na moja wamewasili shuleni.
*Watu wasaba waliangamia katika ajali hiyo.
*Madereva wasita wametiwa mbaroni kwa kosa la kuendesha magari wakiwa walevi.
*Wanafunzi tano wametimuliwa shuleni kwa kuhusika katika mgomo.
*Vitabu nne havina majalada.

Baadhi ya idadi zimetokana na asili za kigeni yalivyo pia maneno mengine ya Kiswahili. Kutoka moja hadi kumi, kuna jumla ya idadi nne ambazo zimetokana na asili ya kigeni. Hizi ni pamoja na sita, saba, tisa na kumi.

Idadi hizi hazichukui viambishi vyovyote. Tunasema watu sita, vitabu sita, vichwa sita, miguu sita, miti sita, nywele sita, nyuzi sita, ndizi sita na kadhalika. Hali hiyo hujirudia katika idadi tisa, saba na kumi. Idadi nyingine ambayo haina viambishi ngeli ni thelathini.

Idadi nyingine zote zilizosalia huchukua viambishi kutegemea ngeli mbalimbali. Kwa hivyo, wanafunzi ni kumi na mmoja wala si kumi na moja; vitabu ni vinne wala si nne; watu watano wala si tano miongoni mwa idadi nyingine.

Alhasili, idadi ni suala la msingi mno katika lugha ya Kiswahili wala halipaswi kupuuzwa katika mawasiliano ya kila siku.