Makala

NDIVYO SIVYO: ‘Katisha’ na ‘katiza’ ni dhana mbili zenye maana tofauti

March 13th, 2019 2 min read

Na ENOCK NYARIKI

KUNA baadhi ya maneno ambayo japo asili yake ni moja, maana huwa tofauti.

Haya ni maneno ambayo miisho yake huchukua sura tofauti za mofu moja.

Kwa mfano, lipisha na lipiza ni maneno mawili ambayo yametokana na kauli ya kutendesha na ambayo yanatofautiana kimaana.

Katika toleo la awali la Kamusi ya Kiswahili Sanifu, maneno hayo mawili yanajitokeza chini ya neno lipa ambalo ndilo chimbuko la maneno yenyewe.

Toleo hilo linaonyesha kuwa neno mojawapo linaweza kuendelezwa kwa njia mbili tofauti. Yaani, mtu anaweza kusema lipiza au lipisha akirejerelea jambo lile lile moja.

Hata hivyo, lipiza na lipisha ni dhana mbili zenye maana tofauti.

Kulipiza ni kumfanyia mtu jambo baya kwa sababu alikufanyia baya jingine mwanzoni. Hivyo ndivyo linavyofafanuliwa kwenye Kamusi Elezi ya Kiswahili.

Kamusi ya Karne ya 21 inaeleza kuwa ni kumfanyia mtu kitendo fulani kwa nia ya kumrudishia ubaya aliokufanyia.

Neno lipisha nalo linafungamana na nomino malipo.

Kamusi ya Karne ya 21 inaeleza kwamba dhana lipisha ina maana ya kumfanya mtu fulani alipe gharama ya kitu alichoharibu au kupoteza.

Maana nyingine ya neno hilo, kwa maoni yangu, ni kumtoza mtu ada fulani kutokana na bidhaa au huduma iliyotolewa.

Maneno mengine ambayo huwakanganya watumiaji na ambayo yatakuwa kitovu cha mjadala wetu ni katisha na katiza.

Katika toleo la awali la Kamusi ya Kiswahili Sanifu, kauli ya kutendesha ya neno kata ni katisha nayo inawakilishwa na mofu {-ish}.

Mofu {-iz} haijitokezi popote katika neno hilo kuwakilisha kauli hiyo.

Hata hivyo, kwenye kamusi hiyo inajitokeza nomino katiza ambayo imepewa fasili mbili changamano mno.

Usafiri. Katuni/ Samuel Muigai

Inaelezewa kuwa ni ukataji wa kitu katikati na uzuiaji wa jambo kabla halijakamilika.

Udhaifu

Hapa unajitokeza udhaifu mmoja unaotokana na mnyambuliko wa kitenzi kata.

Udhaifu wenyewe unatokana na ugumu uliopo wa kuelezea jinsi mofu{-ish} inavyoishia kuchukua umbo {-iz} katika nomino katiza.

Katika kamusi za punde zaidi, “katiza” ni neno linalojisimamia kwenye kamusi.

Kamusi ya Karne ya 21 imelipa fasili tatu.

Kwanza, ni kupita njia ya mkato.

Pili, ni kuacha kuendelea kufanya shughuli au ni kuzuia jambo lililokuwa likifanyika lisiendelee. Tatu, ni kuingilia katika mazungumzo au kudakiza.

Maneno haya, katisha na katiza, sharti yatofautishwe hasa yanapojitokeza katika semi mbalimbali.

Mathalani, mtu humkatiza mwingine tamaa bali si kumkatisha tamaa.

Mawasiliano hukatizwa bali si kukatishwa.

Neno katisha nalo linafungamana sana na kitendo cha kugawa kitu katika sehemu mbili.