Makala

NDIVYO SIVYO: Kiima kinapodhibiti upatanisho, sentensi huepuka utata kisarufi

May 27th, 2020 2 min read

Na ENOCK NYARIKI

MAKOSA matatu hufanywa kila wakati maneno kama vile idadi, maelfu, hadhira n.k. yanapotokea mwanzoni mwa sentensi au kabla ya vitenzi vikuu.

Kwanza, maneno yenyewe hukosa kutekeleza dhima yake katika sentensi. Pili, huibua utata katika sentensi kwa kukosa kulenga kirejelewa. Tatu na muhimu, huikosesha sentensi upatanisho wa sarufi.

Sasa tuzichanganue hoja tatu tulizozitaja kwa kuutumia mfano wa taarifa iliyopeperushwa na kituo kimoja cha habari: Idadi ya visa vya dhuluma za kinyumbani vinazidi kuongezeka wakati huu wa janga la corona.

Neno ‘idadi’ linakosa kutekeleza dhima ambayo limekusudiwa katika sentensi hii kwa kuwa upatanisho wa sarufi wa kinachorejelewa baadaye kwenye sentensi haukubaliani na nomino inayoongoza sentensi ambayo katika muktadha huu ni ‘idadi’.

Kwa kurejelea hoja ya pili, si rahisi kwa anayezungumziwa kuelewa jambo linalorejewa katika sentensi hii kutokana na kubadilika ghafla kwa upatanisho wa sarufi. Je, sentensi inarejelea ‘idadi’ au ‘visa’? Tatu, sentensi haikuzingatia upatanisho wa sarufi. Jambo hili linatokana na matumizi ya kiambishi kinachokinzana na ‘neno kuu’ katika sentensi.

Kiambishi tunachokizungumzia ni {vi} nacho kinajitokeza mwanzoni mwa kitenzi kisaidizi ‘zidi’. Alimradi, hoja zote tatu zinazunguka upatanisho wa sarufi wa neno kuu. Yaani, hatuwezi kusema: *‘idadi vinazidi kuongezeka’!

Kosa la upatanisho wa sarufi linalojitokeza katika sentensi lingeepukwa iwapo mambo yafuatayo yangezingatiwa. Kwanza, kupunguza idadi ya nonimo katika sentensi kwa kutathimini mchango wa kila nomino.

Kwa mfano, sentensi ambayo ni kitovu cha mjadala huu ina nomino tatu ambazo ni: idadi, visa na dhuluma. Nomino ‘dhuluma’ inatekeleza dhima muhimu sana katika sentensi kwa kuwa imebeba mada ya kile kinachozungumziwa. Nomino ‘idadi’ ina umuhimu mdogo katika sentensi kwa sababu maneno ‘zidi’ na ‘kuongezeka’ tayari yanafafanua wingi, ukubwa au uzito wa kinachozungumziwa. Ukibaki na nomino ‘visa’ na ‘dhuluma’ itakuwa rahisi kumakinikia upatanisho wa sarufi wa sentensi kwa kuiendeleza hivi: Visa vya dhuluma za kinyumbani vinazidi kuongezeka wakati huu wa janga la corona.

Pili, kwa kuepuka tafsiri ya moja kwa moja ya baadhi ya kauli kutoka kwa lugha ya Kiingereza. Inawezekana kuwa sentensi hii ingezingatia muundo wa Kiswahili, hata neno visa (cases) lisingekuwa na mchango mkubwa katika kuipa mantiki.

Alhasili, iwapo ni lazima maneno yanayoonyesha hesabu, idadi au takwimu fulani yatumiwe katika sentensi, faradhi upatanisho wa kisarufi wa maneno hayo umakinikiwe ili: kwanza, kuepuka utata katika sentensi na, pili, kutoipotosha kisarufi. Kwa hivyo, sentensi ambayo tumekuwa tukiijadili ingeandikwa hivi: Idadi ya visa vya dhuluma za nyumbani inazidi… Sentensi inarejelea idadi wala si visa.