Makala

NDIVYO SIVYO: Kudhihaki au kudharau mtu ni kumcheka bali si kumchekelea

March 25th, 2020 2 min read

Na ENOCK NYARIKI

VIAMBISHI vya kauli ya kutendea ni {i} , {li}, {e} na {le}.

Viambishi hivi hutokea katika mazingira tofauti tofauti. Kwa mfano, iwapo mzizi una mojawapo ya irabu |a|,|u| au |i|na unaishia kwa konsonanti, kiambishi cha kauli ya kutendea huwa ni {i}. Mfano, vunja huwa vunjia. Ikiwa mzizi una mojawapo ya irabu |e| au |o| na unaishia kwa konsonanti, kiambishi cha kauli ya kutendea ni {e}. Mfano, komboa huwa kombolea.

Kabla ya kufafanua mazingira ambamo mofu {li} na {le} hutokea, nitalitaja kosa ambalo limezoeleka katika mazungumzo ya watu na ambalo tutaliangazia katika makala haya.

Kauli zifuatazo hujitokeza katika mazungumzo: ‘Kwa nini unanichekelea?’; ‘Wacha kumchekelea mwenzako’; Wewe nichekelee tu; ‘Watu walimchekelea mpaka akaaibika’; ‘Wacha kumchekelea mwenzako’. Uhalisia wa mambo ni kuwa lugha ya Kiswahili haina neno *‘chekelea’!

Kiambishi {le} cha mnyambuliko katika kauli ya kutendea hutokea katika mazingira ambapo mzizi una mojawapo ya irabu {e} au {o} na unaishia kwa irabu. Mifano: oa huwa olea; toa huwa tolea; lea huwa lelea.

Mzizi unapokuwa na mojawapo ya irabu |a| , |u| au {i} na unaishia kwa irabu, kiambishi cha mnyambuliko katika kauli ya kutendea huwa ni {li}. Mifano: vua huwa vulia; lia huwa lilia.

Ni muhimu kutaja kuwa sauti [l] ambayo inajitokeza katika {le} na {li} inavunja mfuatano wa vokali ili neno likubali muundo unaopendelewa na lugha za Kibantu . Muundo huo ni ule wa KVKV yaani; konsonanti- vokali, konsonanti- vokali. Inaaminika kuwa sauti hiyo ni sehemu ya muundo wa ndani wa maneno yenyewe.

Muundo wa ndani ndio muundo asilia wa neno. Kwa hivyo, muundo asilia wa neno “zoa” ni *zola; “zaa” ni *zala; “oa” ni *lola; “kaa”ni *kala n.k. Kwa mintarafu hii, sauti [l] inayojitokeza katika neno “kalia’’ , “zalia’’ au zolea ni sauti asilia ya maneno hayo. Sauti hiyo ilikuwepo kabla ya kupitia badiliko la kifonolojia.

Kauli ya kutendea ya kitenzi cheka ni chekea. Kitenzi chekea kina maana ya kufurahia kitu, mtu au hali. Mfano: Juma aliuchekea mshumbi wa wali kwenye sahani yake. Katika kauli ya kutenda, kitenzi cheka huibua dhana mbili muhimu. Kwanza, toa sauti ya furaha kwa kufunua kinywa mpaka meno yakaonekana.

Pili, kumdhihaki au kumdharau mtu. Alhasili, kumdhihaki au kumdharau mtu ni kumcheka bali si kumchekelea jinsi watu wengi walivyozoea kulitumia neno hili.