Makala

NDIVYO SIVYO: Matumizi ya 'chinja' kwa maana ya 'fanyia upasuaji' yana mushkeli

September 11th, 2019 2 min read

Na ENOCK NYARIKI

KUNAZO sababu kadha ambazo yamkini huwafanya watu kuyafasili maneno ya Kiswahili visivyo.

Kwanza, baadhi ya maneno katika lugha za kwanza za watu hao na yale ya Kiswahili hufanana sana kimaendelezo hivi kwamba ni rahisi kuyakanganya.

Kwa mfano, mzawa wa Kisii anaweza kuuita msuli “mkia” kwa sababu fasiri ya dhana msuli katika lugha hiyo ni “omokia”.

Pili, baadhi ya dhana hufasiriwa moja kwa moja kutoka lugha za kwanza hadi lugha ya Kiswahili.

Kwa mfano, katika jamii ya Kikuyu, “kutoa” na “kufanya” ni maneno mawili yanayokurubiana mno hivi kwamba si ajabu kumsikia mzawa wa jamii hiyo akisema “mke wangu ‘anatoa’ kazi” kwa maana ya “mke wangu anafanya kazi”.

Hakika, jinsi dhana hizo zinavyoeleweka katika lugha ya kwanza ndivyo zinavyohawilishiwa lugha ya Kiswahili.

Sababu nyingine ambayo inakaribiana sana na hiyo ya pili ni kwamba baadhi ya dhana zinaweza kuwa na maana zaidi ya moja katika lugha fulani.

Maana hizo huhawilishwa vivyo hivyo hadi lugha ya Kiswahili hata pale ambapo mojawapo ya dhana haileti mantiki katika lugha ya pili.

Kwa mfano, katika lugha ya Kikuyu, hapana tofauti kati ya kumchinja mnyama na kumfanyia binadamu operesheni. Hakika nimewahi kuwasikia watu wengi kutoka jamii hiyo wakisema kwamba fulani alichinjwa wakati wa kujifungua wakiwa na maana kuwa alifanyiwa operesheni au upasuaji.

Licha ya kwamba dhana “chinja” kwa maana ya fanyia operesheni si sahihi katika mazingira hayo, dhana yenyewe ina makali yanayoifanya kuogofya.

Hakika, operesheni ni utohozi wa neno la Kiingereza “operation”.

Hata hivyo, hii haina maana kwamba lugha za Kibantu au Kiswahili zimetindikiwa na msamiati ambao unaweza kutumiwa kuelezea kitendo chenyewe.

Neno upasuaji, kwa mfano, ni dhana faafu inayoweza kutumiwa.

Hata hivyo, baadhi ya misemo hii sharti iandamane na maneno mengine ambayo husaidia katika kuipa tasfida na kupunguza makali ambayo yangezuka endapo ingetumiwa peke yao.

Mathalani, haiyumkiniki kusema kwamba fulani amepasuliwa kwa sababu neno hilo lina makali sawa na hayo yanayoletwa na neno “chinja”. Hata hivyo, tunaposema kwamba fulani amefanyiwa upasuaji, neno “fanyiwa” linasaidia katika kukisanifisha kitendo chenyewe.

Alhasili, neno “kuchinja” halipaswi kutumiwa kwa maana ya upasuaji unaofanyiwa mgonjwa kama tiba. Kuchinja ni kukata shingo au sehemu ya mwili wa mnyama au binadamu.

Maana ya pili ya neno lenyewe ni kupunja au kuibia mtu katika vipimo vya uzito. Neno mwafaka ambalo linapaswa kutumiwa kuelezea kitendo hicho cha kimatibabu ni kufanyia operesheni au upasuaji.