Makala

NDIVYO SIVYO: Mkanganyiko unaoibuliwa na maneno 'ganda' na 'gome'

March 11th, 2020 2 min read

Na ENOCK NYARIKI

MANENO gome na ganda hutumiwa aghalabu kwenye sehemu za mashambani kunakokuzwa miti na mimea mingine kama vile miwa, migomba na michungwa.

Licha ya kuwa matumizi ya maneno hayo yamesheheni kwenye sehemu hizo, si watu wengi wanaoweza kuyatofautisha. Majuzi niliwasikia watu fulani waliokuwa wakijenga nyumba wakisema, “Ondoa maganda kwenye fito kabla ya kuzitumia.’’ Sentensi hii ina makosa mawili. Kosa la kwanza linatokana na matumizi ya neno ondoa; ingawa hakika neno hilo linapotumiwa hivyo katika lugha ya ‘barabarani’ hueleweka. Neno mwafaka ambalo lingetumiwa ni babadua.

Neno babadua ambalo linaweza pia kuendelezwa au kutamkwa kama babatua lina maana mbili ila tutaitaja tu maana inayohusiana na mjadala huu: kuachanisha vitu vilivyoshikamana kama maganda ya mti. Maelezo haya ni kwa mujibu wa Kamusi ya Karne ya 21.

Jambo moja ambalo ni muhimu kulimakinikia kwenye maelezo hayo ni matumizi ya neno ‘maganda’. Maneno ganda na gome yanatofautiana kimaana ingawa watu huyakanganya katika mawasiliano.

Jambo hilo yamkini linatokana na sababu mbili. Sababu ya kwanza ni kuwa hizi ni sehemu za nje za mimea au matunda ya mimea zenye sifa zinazofanana na zinazotekeleza kazi sawa. Sababu ya pili inatokana na kujirudiarudia kwa neno mojawapo katika ufafanuzi wa jingine. Neno gome linaelezewa kuwa ni ganda la mti. Neno hili la pili linajirudia pia katika kauli kama vile ganda la yai, kiberiti n.k.

Kutumiwa kwa neno ganda kulifafanua gome kunayafanya maneno haya mawili kuwa na uhusiano wa kifahiwa wa aina fulani hivi kwamba neno moja linaweza kutumiwa kwenye nafasi ya jingine. Hata hivyo, ni muhimu kufahamu kuwa sehemu ya nje ya mmea ambayo inaweza pia kutumiwa kama kamba ya kufungia vitu ni gome bali si ganda. Ganda ni kwa mua, tunda n.k. Ganda la yai au kiberiti huitwa kaka. Hata hivyo, gamba tupu la kiberiti ni galasha.

Katika maelezo ya hapa juu tumelitaja neno gamba ambalo kimatamshi linakaribiana na ganda. Ijapokuwa neno la kwanza hutumiwa hasa kueleza kitu kama plastiki kinachoota juu ya mwili wa samaki, ndege au mnyama, pia hujumlisha vitu vingine vyenye maumbo na sifa zinazofanana na kitu chenyewe. Kwa mfano kuna gamba la kiberiti, mgomba na kitabu. Gamba la mgomba lililokauka huitwa sago.

Alhasili, ijapokuwa maneno gamba na gome hukanganywa katika mawasiliano, yanatofautiana. Gome ni sehemu ya nje ya mti ambayo inapobabaduliwa inaweza kutumiwa kufungia vitu kama vile kuni.