Makala

NDIVYO SIVYO: Si ustaarabu kumwita baba buda, huko ni kumtweza mzazi

June 19th, 2019 2 min read

Na ENOCK NYARIKI

KIJILUGHA cha Sheng ambacho ni maarufu miongoni mwa vijana kina namna fulani ya kuyachukua maneno ya Kiswahili na kuyapa maana inayokaribiana au yenye uhusiano fulani na maana ya msingi ya maneno yenyewe.

Mfano mzuri wa maneno hayo ni “jali” ambalo kimuundo linakaribiana na neno rijali.

Hata hivyo, neno la kwanza lina maana tofauti na ile ambayo vijana hulinasibisha nayo. Maana ya msingi ya neno jali ni kutia maanani au kuthamini na kumhudumia mtu ipasavyo.

Hata hivyo, lugha ya mtaani hulitumia neno hilo baada ya kuligeuza na kuita “chali” kwa maana ya kijana mwanamume au rafiki wa kiume wa msichana au mwanamke.

Ni sadfa tu kwamba neno lenye maana inayokaribiana na ile ya kilugha hicho cha mtaani ni rijali.

Neno rijali lina maana ya mwanamume mwenye uwezo wa kusimika au kuzaa.

Kusimika ashakum si matusi ni kusimama kwa uume. Msemo wa Kiswahili unaotumiwa kumrejelea mwanamume ambaye hana uwezo wa kusimika ni “jongooo hapandi mtungi”.

Ijapokuwa neno “jali” linavyotumiwa na vijana wa kike kwa kiume kwa maana ya kijana mwanamume au rafiki wa kiume wa mtu haliafiki kabisa maana ya msingi ya rijali, kunao uhusiano wa namna fulani; ule wa mwanamume.

Waama, kunayo maneno kadha ya Kiswahili ambayo kwa namna fulani hukaribiana katika maana ya msingi na Sheng’.

Si lengo letu kuyaangazia maneno yenyewe katika safu hii maadamu nafasi haipo.

Katika makala haya, tutaliangazia neno “buda” ambalo matumizi yake yameenea sana katika lugha ya mtaani kuliko ilivyo katika Kiswahili sanifu.

Vijana hulitumia neno buda kwa maana ya baba ila tutakavyoona baadaye limepanua maana yake. Kutoka kwenye neno “mbuyu” ambalo vijana walilitumia kwa maana ya baba, waliligeukia jina “buda” kwa maana hiyo.

Hata hivyo, Sheng’ imeanza kulitumia jina “buda” kwa maana ya kijana au mwanamume yeyote mwenye umri wa makamo.

Aghalabu, vijana wa kiume huitana kwa jina hilo – wenyewe kwa wenyewe – wanapohimizana kuhusu jambo fulani.

Jina buda hata hivyo lina maana ya mwanamume aliyezeeka sana au kibogoyo.

Maana yake nyingine ni ndovu aliyezaliwa bila pembe ua ndovu ambaye hana pembe.

Alhasili, sidhani kwamba kuna kijana yeyote ambaye angependa kumkosea baba yake heshima kwa kumwita kibogoyo au ‘mwanamume mzee sana’ au ‘ndovu ambaye hana pembe’; hasa iwapo baba mwenyewe ni mtu wa makamo na mwenye nguvu zake. Neno buda litumiwe kwa maana yake ya msingi.