Makala

NDIVYO SIVYO: Tafsiri ya Kiingereza ya ‘it doesn’t matter’ ni ‘si hoja’

September 9th, 2020 2 min read

Na ENOCK NYARIKI

BAADHI ya watu hulitumia neno ‘haijalishi’ kwa maana ya si neno au si hoja.

Hakika neno hilo aghalabu hutumiwa kujiliwaza kwamba tusijisumbue sana na jinsi hali ilivyo katika wakati fulani au tusiyazingatie sana masaibu tunayoyapitia sasa kwani si ya kudumu.

Uhalisia wa mambo hata hivyo ni kwamba hiyo si maana sahihi ya neno hilo ingawa ‘lugha ya barabarani’ imeithamini sana. Matumizi haya yanatokana na tafsiri potovu ya Kiingereza ya ‘it doesn’t matter’.

Jalisha ni kauli ya kutendesha ya kitenzi elekezi ‘jali’ chenye maana mbili kuu. Kabla ya kuzidadavua maana hizo, ni muhimu kueleza kwamba kitenzi elekezi ni kile ambacho hufuatwa na yambwa. Kinyume cha kitenzi elekezi ni kitenzi si elekezi. Sasa tufafanue maana mbili za jali.

Kwanza, ni kutia maanani au kusikiliza. Mfano: Usiyajali sana maneno aliyoyatamka kwa ujeuri kwenye kikao cha juzi. Maana ya pili ya neno hilo ni kuheshimu, kutii au kustahi. Mfano: Juma Jeuri anawajali sana wenye hadhi katika jamii. Kitenzi jali kinaponyambuliwa katika kauli ya kutendesha, huwa na maana hizo tulizozitaja ila katika kauli husika.

Mathalani, tunaweza kuuandika mfano tulioutaja katika maana ya kwanza hivi: Maneno aliyoyatamka kwa ujeuri kwenye kikao cha jana yasikujalishe. Katika sentensi hii, kauli ‘yasikujalishe’ ina maana ya usiyatie maanani au yasikufanye kujisumbua.

Si kauli zote za Kiingereza ambazo zinaweza kupata maana ya moja kwa moja katika lugha ya Kiswahili. Baadhi ya kauli zitajipambanua vyema katika miktadha ya matumizi. Mfano mzuri ni ‘meet somebody’s needs’ ambao tulieleza kwamba una maana ya kumtimizia mtu haja au mahitaji bali si kukutana na mahitaji ya mtu.

Kauli ‘it doesn’t matter’ nayo inapaswa kutafsiriwa kuwa si hoja au si neno. Kwa hivyo, iwapo nia ya msemaji ni kujiliwaza au kumliwaza mwenzake kutojitaabisha sana na jinsi hali ilivyo, basi anapaswa kusema: Si hoja kwamba janga la corona limesababisha ugumu wa maisha kwani kuna matumaini ya siku za halafu.

Alhasili, haijalishi si matumizi rasmi ya ‘isiwe hali inayosababisha udhia sasa au lisiwe jambo linalomfanya mtu kuzama katika bahari ya mawazo isivyo lazima. Usemi ambao unapaswa kutumiwa kwa maana hiyo ni ‘si hoja’ au ‘si neno’.