NDIVYO SIVYO: Ukanushi wa kitenzi kishirikishi kipungufu ‘ni’ ni ‘si’ wala si ‘sio’!

NDIVYO SIVYO: Ukanushi wa kitenzi kishirikishi kipungufu ‘ni’ ni ‘si’ wala si ‘sio’!

Na ENOCK NYARIKI

SIO si ukanushi wa kitenzi ‘ni’.

Tazama jinsi nilivyolitumia neno “si” baada ya “sio”.

Vinginevyo, ningeshawishika kusema: ‘…kitenzi kikanushi sio ‘sio’ ukanushi wa kitenzi’.

Nitairejelea kauli hii ili kuifafanua zaidi ila kwanza ni muhimu kueleza kuwa ‘ni’ ni kitenzi kishirikishi kipungufu.

Dhana vitenzi vishirikishi hutumiwa kwa maana ya vitenzi vinavyoshirikisha vitu mbalimbali kihali, kitabia au kimazingira.

Navyo vitenzi vishirikishi vipungufu haviwezi kuchukua viambishi vya wakati ingawa hakika vinaweza kuchukua viwakilishi nafsi-viambata na viambishi ngeli.

Kinyume cha vitenzi vishirikishi vipungufu ni vitenzi vishirikishi vikamilifu. Mahali fulani hapa juu tumetaja dhana ‘viwakilishi nafsi-viambata’.

Dhana hii itaeleweka vyema baada ya kufafanua maana ya ‘viwakilishi nafsi’.

Viwakilishi nafsi ni maneno kamili au viambishi vinavyosimamia nomino za viumbe vyenye uhai hususan binadamu.

Mimi, wewe, yeye ni viwakilishi nafsi huru kwa kuwa ni maneno yanayojisimamia na yanayoleta maana ilhali ‘ni-’, ‘u-’, ‘a-’ ni viwakilishi nafsi-viambata kwa sababu haviwezi kuleta maana mpaka vitumiwe au kufuatwa na maneno mengine.

Ukanushi wa sentensi “Mimi ni daktari wa mifugo” si “*Mimi sio daktari wa mifugo”.

Tena tazama matumizi ya ‘si’ – ambayo imetangulia kiwakilishi nafsi huru ‘mimi’. ‘Sio’ ni wingi wa ‘siye’. Maneno yote mawili yaani; siye na sio, yako katika hali kanushi.

Siye ni ukanushi wa kitenzi kishirikishi kipungufu ndiye.

Kwa mfano, ukanushaji wa sentensi, “Yeye ndiye aliyetuletea habari hizo’’ ni “Yeye siye aliyetuletea habari hizo’’.

Ningependa kueleza kwamba si kosa kutumia ndi- pamoja na O-rejeshi katika sentensi moja.

Kosa hilo litatokea iwapo mzizi amba- utatumiwa pamoja na O-rejeshi katika sentensi moja.

Hata hivyo, pasi na kutumia kiwakilishi nafsi huru katika sentensi tuliyoitaja hapa juu, bado maana itajitokeza wazi.

Pengine athari ya pekee itakayojidhihirisha ni kuondolewa kwa msisitizo. Kwa njia nyingine, tunaweza kusema: ‘Ndiye aliyetuletea habari hizo’ – sentensi hii ikawa na maana sawa na ile tuliyoitaja hapo juu.

Siyo nao ni wingi wa silo. Kwa mfano, sentensi “Jambo hili silo nililolitarajia’’ katika wingi itakuwa “Mambo haya siyo tuliyoyatarajia.”

‘Sivyo’ ni neno linalotumiwa kupinga kilichosemwa. Mfano: ‘Hivi sivyo ulivyotuambia jana’.

Neno hilo pia ni wingi wa ‘sicho’. Alhasili, ukanushi wa kitenzi kishirikishi kipungufu ‘ni’ ni ‘si’ bali si ‘sio’ jinsi baadhi ya watu wanavyokitumia.

Tunasema: Yeye si mjinga; Mimi si daktari; Hili si jibu sahihi; bali si: *Yeye sio mjinga; *Mimi sio daktari na kadhalika.

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Dennis Mwima

SAUTI YA MKEREKETWA: Sekta ya elimu nchini itafaidi iwapo...