Makala

NDIVYO SIVYO: Usiseme ‘nimekukosa’ badala yake sema kuwa ‘nimekupeza’

March 6th, 2019 2 min read

Na ENOCK NYARIKI

PALE ambapo hapana neno moja linaloweza kutumiwa kueleza dhana fulani kwa Kiswahili, watu hushurutika kutumia maneno mengi kufanya hivyo.

Kwa wale ambao daima wamezoea kutumia njia za mkato kuwasilisha ujumbe, huyagagamiza maneno ili kufanikisha lengo lao bila kujali wala kubali iwapo maneno ambayo ni zao la njia hizo za mkato ni sahihi au la.

Kwa hivyo, mara nyingi utawasikia watu wakisema “tumepoteanwa” wakiwa na maana kwamba “hatujaonana kwa muda mrefu”.

Neno hilo “poteanwa’’ hudhaniwa kuwa fasiri ya “miss each other”. Wengine husema: “umenipotea” kwa maana ya “I have missed you”.

Vyovyote iwavyo, tafsiri za neno hilo la Kiingereza zimelemaa na zimefanikiwa tu katika ‘mawasiliano ya barabarani’.

Yamkini ugumu wa kuitafsiri kauli “I missed you” unafungamana sana na utamaduni wa lugha za Kiafrika.

Sidhani kwamba lipo neno faafu katika lugha hizo linaloweza kutumiwa kukielezea kitendo cha kutamani kuonana na mtu baada ya kutengana naye kwa muda mrefu.

Katika utamaduni wa Kiafrika, kauli “I missed you” pengine ilidhaniwa kuibua hisia fulani hususani hisia za mapenzi, hivyo basi watu hawakuwa radhi kuitumia hata pale ambapo zilikuwapo hisia za “kukosana”.

Nimelitumia neno “kukosana” ambalo ni kauli ya kutendana ya kitenzi “kosa”. Katika wimbo Christina wa Habel Kifoto na Maroon Commandos limetumiwa neno “nimekukosa’’ katika kibwagizo kwa fasiri ya “I have missed you”.

Hivi ndivyo wanavyosema:

Siku gani dada
Utakuja
Nikungojee
Stesheni…..
Nimekukosa
Mama
Nimekukosa
Siku nyingi.

Habel Kifoto amekopa neno “nimekukosa” na utamaduni wake kutoka lugha ya Kiingereza.

Neno lenyewe linakinzana na utamaduni ambao wimbo wenyewe umeimbwa – utamaduni wa Kiafrika – na huenda halijafanikiwa kuziwasilisha hisia zilizolengwa.

Waama, hakuna neno moja katika lugha za Kiafrika linaloweza kuelezea hisia anazokuwa nazo mtu anapokosa kuonana na mwenzake kwa muda mrefu. Hisia zipo ila neno halipo!

Fasili

Katika kamusi za awali, haipo fasiri ya neno “miss’’ kwa maana tuliyoiangazia hapa.

Hakuna fasili yoyote ya kitenzi kosa – kati ya zile zilizotolewa katika toleo la awali la Kamusi ya Kiswahili Sanifu – inayoelezea kitendo cha kutamani kumwona mtu baada ya kutengana naye kwa muda mrefu.

Hata hivyo, katika kamusi za punde zaidi, neno peza linaelezwa kuwa ni kutamani kumwona mtu baada ya kutengana kwa muda mrefu au kuona kitu kwa kukikosa kwa muda mrefu.

Kile siwezi kueleza kwa yakini ni utaratibu uliotumiwa kuliunda neno hili. Linakidhi matilaba? Basi!