Ndoa ya BBI yaingia doa

Ndoa ya BBI yaingia doa

Na WAANDISHI WETU

MVUTANO kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga ulizidi kuchacha Jumatatu, hali iliyolazimisha kuahirishwa kwa sherehe za leo Jumanne za kuadhimisha miaka mitatu ya handisheki.

Pia mkutano wa ushauriano uliopangwa kufanyika leo Jumanne wa viongozi wakuu wa BBI, magavana na wabunge uliahirishwa baada ya joto kati ya wahusika hao kupanda baada ya chama cha ODM kulalamika kuwa kinahujumiwa.

Hii imesababishwa na mvutano kati ya viongozi wakuu wanaounga mkono mchakato wa BBI kuhusu ni nani kati yao anayefaa kumrithi Rais Uhuru Kenyatta wakati atakapoenda nyumbani mwaka ujao.

Kundi hilo la wakuu wa BBI linaongozwa na Rais Kenyatta na linajumuisha Bw Odinga, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi, Moses Wetangula, Gideon Moi na Charity Ngilu.

Lakini sasa muungano huo unayumbayumba siku chache tu baada ya kubuniwa, hali inayotishia mchakato wa BBI, huku ODM kikidai hila ya maafisa wakuu serikalini kuhujumu Bw Odinga kwa ajili ya kumwangusha 2022.

Jumatatu, rafiki wa karibu wa Bw Odinga, Bw Junet Mohamed ambaye pia ni mwenyekiti-mwenza wa makao makuu ya BBI, alidai kuwa kuna njama kubwa zaidi ya kuvuruga ODM na kukiacha vigae ifikapo mwaka 2022.

Bw Mohamed alisema iwapo njama hiyo haitakomeshwa watachukua hatua kuhusu handisheki na BBI.

“Tunajua kuhusu mpango mkubwa wa kudunisha ODM mashinani kwa visingizio vya ushirikiano wa handisheki na BBI. Wabunge na magavana katika ngome zetu za Pwani, Magharibi na Nyanza wanahangaishwa na maafisa wakuu serikalini lakini hatutakubali haya,” akasema Bw Mohamed.

Kulingana na Bw Mohamed, lengo la kutikisa ODM ni kuhakikisha hakitakuwa na nguvu ifikapo uchaguzi wa 2022.

Mnamo Jumamosi, Seneta James Orengo wa Siaya alitisha kuwa ODM kitajiondoa kutoka handisheki na BBI iwapo baadhi ya maafisa wakuu serikali wataendelea kukihujumu.

Matamshi yake ambayo yalionekana kumlenga Katibu wa Wizara ya Usalama, Dkt Karanja Kibicho, yameibua cheche za majibizano ambayo sasa yanatishia kuporomosha maazimio ya Rais Kenyatta na Bw Odinga kuleta upatanisho wa viongozi wa kisiasa kupitia kwa BBI.

Katika hatua ambayo inaharibu zaidi muungano wa BBI na handisheki, chama cha ANC jana kilishambulia ODM kikisema malalamiko yake yamesababishwa na uchoyo wa viongozi wa chama hicho, ambao wanataka kusimamia raslimali zote za kuhamasisha umma kuhusu BBI.

Msemaji wa Bw Mudavadi, Kibisu Kabatesi alidai ODM kinataka kumiliki mpango mzima wa BBI bila kuhusisha vyama vingine vya kisiasa.

“Kile ambacho ANC kinaweza kufanya ni kuonya vyama vingine visilazimishwe katika uhusiano unaoendeshwa kwa msingi wa vitisho na siasa za kushikana mateka,” akasema Bw Kabatesi.

Kwa upande mwingine, viongozi wa Wiper walimwambia Bw Odinga avunje handisheki na Rais Kenyatta ikiwa haridhiki.

Viongozi hao walisema Bw Musyoka ana uwezo wa kuchukua nafasi ya Bw Odinga katika handisheki bila tatizo.

“Nikikualika nyumbani kwangu hufai kuja kuanza kuniagiza jinsi ninavyofaa kupika chakula changu. Hilo haliwezekani. Kama ODM haijaridhishwa, acha waondoke,” Seneta wa Kitui, Enock Wambua akasema.

Jumatatu, Bw Kabatesi alisema kulingana na ufahamu wao, mkutano uliopangwa kufanyika leo Jumanne kuhusu BBI ungalipo licha ya malalamishi yaliyotolewa na ODM kuhusu usimamizi wa BBI na urithi wa Rais Kenyatta.

Mnamo Jumapili, Bw Odinga alikosa kuhudhuria mkutano wa hadhara katika uwanja wa Kamukunji, eneobunge la Kibra, hatua ambayo wadadisi wa kisiasa walihusisha na uadui ambao umeibuka kuhusu usimamizi wa BBI.

Ripoti ya Charles Wasonga, Justus Ochieng na Valentine Obara

You can share this post!

Nafuu Dortmund baada ya Haaland kupona kabla ya mechi dhidi...

Dalili Klopp yuko karibu kuagana na Liverpool