Habari Mseto

Ndoa ya Manu Chandaria na mkewe Aruna sasa ni rasmi baada ya kuishi pamoja miaka 64

July 20th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

MFANYABIASHARA tajiri Manu Chandaria mnamo Ijumaa, Julai 19, 2019, alichukua hatua ya kuifanya ndoa yake na mkewe iwe rasmi na kama kawaida ya watumiaji mitandao ya kijamii, hawakuchelewa kutoa maoni yao.

Chandaria, 90, na Aruna Chandaria, 85, walihalalisha ndoa yao katika afisi ya Mwanasheria Mkuu jijini Nairobi.

Kulingana na picha yao wakiwa pamoja, ni dhahiri kwamba mapenzi yao yangali moto wa kuotea mbali hata baada ya kuishi pamoja kwa muda wa miaka 64.

Kinyume na matarajio ya wengi, Bw Chandaria ambaye ni miongoni wa vigogo wa biashara nchini, hakuandaa harusi ya kifahari na badala yake alifanya sherehe ndogo.

Baadhi ya watumiaji mitandao ya kijamii waliofuatilia tukio hilo kwa karibu walimpongeza bilionea huyo huku wengine wakizua mjadala kuhusu ni kwa muda gani wanandoa au wapenzi wanapaswa kuchumbiana kabla ya kufanya uhusiano wao kuwa rasmi.

Hebu tazama baadhi ya maoni yao kwenye mtandao wa Twitter:

“Nilipoona Manu Chandaria akitanda nilifikiria ameaga dunia lakini ole wangu, kumbe kijana alikuwa tu amefunga ndoa baada ya kuchumbiana na ampendaye kwa miaka 64. Nakuambia amewekea mtoto wa kiume viwango vipya. Wengine huenda wakachumbiana hadi kwa kipindi cha miaka 70,” aliandika Kalydia.

Mwingine,  Lastborn Kanyi, aliandika kuhusu gharama.

“Manu Chandaria ameweka viwango vipya baada ya miaka 64 na Sh9,700. Nisisikie kuhusu makundi ya WhatsApp ya kamati za harusi,” alisema Lastborn Kanyi.

Naye Tony YM aliandika: “Mpendwa Manu Chandaria, maadamu umenipa changamoto, nimefutilia mbali kamati ya harusi yangu. Akiamua (mchumba) hatupaswi kwenda kwa AG nitajipa shughuli.”

Naye mtumiaji mwingine wa mitandao ya kijamii kwa jina Gachoki, alitoa maoni kwamba naye haoni haja ya kuandaa bajeti kubwa.

“Ikiwa harusi ya Manu Chandaria inagharimu chini ya Sh10,000, mimi ni nani niwe na bajeti kubwa kumshinda? Vipi? Wanaume chukueni uhuru wenu. Natumai mke wangu hataona ujumbe huu,” alisema mwingine kwa jina Gachoki.

Mtumiaji mwingine naye alishangaa ni vipi mpenzi ambaye wamekuwa pamoja kwa kipindi cha wiki tatu anamuambia ana mchezo.

“Nimeambiwa nina mchezo kwa kusema tutafunga ndoa Septemba,” aliandika Isaac Nandwa.