Ndoa ya Mudavadi, Ruto yachanganya wawaniaji Magharibi

Ndoa ya Mudavadi, Ruto yachanganya wawaniaji Magharibi

BENSON AMADALA na SHABAN MAKOKHA

HATUA ya kiongozi wa ANC, Bw Musalia Mudavadi na mwenzake na Ford Kenya, Seneta Moses Wetang’ula (Bungoma), kujiunga na chama cha UDA, imewaacha baadhi ya wawaniaji katika eneo la Magharibi kwenye njia panda.

Wawaniaji hao ni wale waliolenga kutumia vyama hivyo kuwania nyadhifa tofauti za kisiasa kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti.

Baadhi ya wawaniaji walikuwa wamehama kutoka chama kimoja hadi kingine kabla ya vyama hivyo kutangaza kuungana.

Mabwana Mudavadi na Wetang’ula walitangaza kushirikiana na chama cha UDA, chake Naibu Rais William Ruto Jumapili, kwenye hafla ambapo ANC ilimwidhinisha Bw Mudavadi kuwania urais Agosti.

Haijabainika ikiwa vyama hivyo vitawasimamisha wawaniaji pamoja au vitazingatia umaarufu wa chama katika eneo husika.

Aliyekuwa Seneta wa Kakamega, Dkt Boni Khalwale alihama kutoka Ford-Kenya hadi UDA, huku mbunge Malulu Injendi (Malava) akitangaza kuhama kutoka UDA na kujiunga na ANC.

Wakati Bw Mudavadi alitangaza kujiunga na kambi ya Dkt Ruto, Dkt Khalwale alisema kuwa kigogo huyo anapaswa kukoma kuipotosha jamii ya Abaluhya kuhusu nia yake kuwania urais.

“Bw Mudavadi anapaswa kukoma kuidanganya jamii ya Abaluhya. Anapaswa kuamua mara moja kumuunga mkono Dkt Ruto kuwania urais, kwani hilo litamwezesha kuwa katika serikali ijayo. Kwa sasa, kigogo huyo hawezi kujifanya ana nafasi yoyote kushinda urais,” akasema Dkt Khalwale.

Mwanasiasa huyo ametangaza atawania ugavana katika Kaunti ya Kakamega kwa tiketi ya UDA, huku Bw Injendi akitetea nafasi yake kwa tiketi ya ANC.

Hali hiyo huenda ikaathiri mipango yao ya kisiasa, kwani wamelazimika kungoja mwelekeo utakaotolewa na wakuu wa vyama hivyo.

Vyama vya ANC na Ford-Kenya vina uungwaji mkono mkubwa katika eneo la Magharibi, huku UDA ikionekana kuwa na uungwaji mkono katika sehemu tofauti kote nchini.

ANC ina ufuasi mkubwa katika kaunti za Vihiga na Kakamega huku Ford-Kenya ikiwa na wafuasi wengi katika kaunti za Bungoma na Trans Nzoia.

Ikiwa vyama hivyo vitatu vitaungana chini ya Muugano wa Kenya Kwanza, basi huenda wawaniaji wengi wakakosa nafasi kuwania nyadhifa wanazolenga.

Katika Kaunti ya Kakamega, ushindani mkali unatarajiwa kati ya Dkt Khalwale na Seneta Cleophas Malala, ambapo wote wanalenga kuwania ugavana.

Dkt Khalwale ametangaza atawania kwa tiketi ya UDA huku Bw Malala akitangaza kuwania kwa tiketi ya ANC.

Katika Kaunti ya Bungoma, Bw Zachary Barasa ametangaza kuwania ugavana kwa tiketi ya UDA dhidi ya Gavana Wycliffe Wangamati na Spika wa Seneti Ken Lusaka.

Bw Wangamati alichaguliwa mnamo 2017 kwa tiketi ya Ford-Kenya lakini akahamia katika chama kipya cha Democratic Action Party-K (DAP-K) kinachohusishwa na Waziri wa Ulinzi, Eugene Wamalwa.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Badi asije akasahau kuwa karibu hospitali...

Issa Boy azidi kupata ushindani

T L