Michezo

Ndoa ya mwanavikapu aliyerambishwa asali ya wizi sasa inayumba

November 12th, 2018 1 min read

NA MWANDISHI WETU

ALIYEKUWA nyota wa NBA, Marcus Camby yuko katika hatari ya kusalia mpweke baada ya kushtakiwa kwa kosa la kumtelekeza mtoto ambaye ni zao la jicho lake la nje.

Kwa mujibu wa kipusa Noemi Valdez, Camby ndiye baba wa Makiah, mtoto wa kike mwenye umri wa miaka saba aliyepatikana katika uhusiano wa siri uliodumu kwa kipindi cha mwaka mmoja mnamo 2010.

Akimtaka Camby aliwajibikie zao la miereka waliyoicheza faraghani wakati huo, Noemi kwa sasa ameelekea kortini kwa sababu mbili.

Mosi, anamtaka Camby asiwe na mazoea ya kuonana na mtoto Makiah popote na vyovyote apendavyo. Pili, analitaka dume hilo liwe likimpokeza kima cha Sh80 milioni kila mwezi ili kuyakimu mahitaji ya kimsingi ya Makiah.

Kulingana na gazeti la The Blast nchini Amerika, stakabadhi zote za korti zinaonesha kwamba Makiah alizaliwa mnamo 2011 na Camby hakupinga suala la uzazi.

Mnamo 2012, Noemi alipakia katika mitandao yake ya kijamii picha nyingi alizopigwa kwa pamoja na mwanavikapu huyo pamoja na Makiah katika sehemu mbalimbali za burudani.

Katika mojawapo ya picha, videge hao walipania kudhihirisha ukomavu wa penzi lao kwa kupigana mabusu motomoto mashavuni wakati wakiadhimisha mwaka mmoja wa kuzaliwa kwa mwanao Makiah.

Katika wasilisho lake mahakamani, Noemi anakiri kwamba alishawishika kutoka kimapenzi na Camby kwa kuwa alimsisitizia kwamba alikuwa kapera.

“Nilianza kumfungulia buyu la asali aliponisadikisha kwamba hakuwa na mke wala katika uhusiano wowote mwingine wa kimapenzi,” asema Noemi.

Ilikuwa hadi 2013 ambapo Camby alitemana na Noemi aliyegundua kwamba nyota huyo wa basketiboli ana mke aitwaye Eva ambaye kwa pamoja wamejaliwa watoto wawili. Camby alifanya Eva kuwa wake wa halali mnamo 2008 katika harusi iliyohudhuriwa na wanavikapu maarufu wa NBA.