HabariSiasa

Ndoa ya ODM na Jubilee yaingia doa

July 6th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

KUJIVUTA kwa chama cha ODM, kukubali mkataba wa ushirikiano na chama cha Jubilee kulisababisha mzozo kuhusu uanachama wa kamati tatu za bunge ambazo ni muhimu katika utekelezaji wa ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI), imebainika.

Kwenye mkutano ulionuiwa kugawana nafasi za kamati zilizoachwa wazi baada ya wandani wa Naibu Rais William Ruto uliofanyika mwishoni mwa wiki jana, Jubilee ilikataa wito wa ODM wa kutaka kitengewe nafasi katika kamati hizo.

Kiongozi wa wengi Amos Kimunya na Naibu Mwenyekiti wa chama cha Jubilee David Murathe waliambia ODM kuridhika na nafasi walizotengewa.

Bw Kimunya aliambia ODM kwamba orodha hiyo ilikuwa imeidhinishwa na Rais Uhuru na hakuwa na uwezo wa kuibadilisha kamwe.

Kulingana na Bw Murathe, ODM inafaa kukubali orodha ya Jubilee akisema chama hicho hakina haki ya kudai nafasi zaidi.

“Hakuna cha kushauriana kuhusu orodha hii. Rais anajua uwezo wa kila mbunge na aligawa viti hivyo kwa kutegemea kigezo hicho. Isitoshe hauwezi kuamua kamati ambayo unataka kuhudumu,” Bw Murathe alisema.

Lakini kulingana na mwenyekiti wa ODM John Mbadi mkutano huo ulikuwa wa kuamua wanachama wa kamati za haki na sheria, kamati ya bajeti na kamati teule kuhusu sheria.

Nafasi hizo zilibaki wazi baada ya wandani wa Ruto; William Cheptumo, Gladys Shollei na Kimani Ichungwa kutemwa. Watatu hao walikuwa miongoni mwa wandani wa Dkt Ruto waliopokonywa nyadhifa za uongozi bungeni kwa kukosoa handisheki na BBI. Baada ya kutimuliwa kwao, ODM kilisema kilifaa kutengewa uongozi wa baadhi ya kamati hizo ambazo ni muhimu katika utekelezaji wa BBI bungeni.

Kwenye mkutano huo wabunge wa ODM walidai kwamba wandani wa Ruto walitengewa nafasi katika kamati hizo na wangehujumu ripoti ya BBI itakapowasilishwa bungeni.

Kulingana na mdadisi wa siasa John Okumu, huenda Jubilee inachezea ODM kwa kukataa kutia mkataba wa ushirikiano zilivyofanya vyama vya Kanu, Wiper na Chama cha Mashinani (CCM) au kuna juhudi za kuyumbisha mchakato wa BBI na handisheki kwa njia moja au nyingine.

“Huu ulikuwa ujumbe kwa ODM kwamba kunafaa kufuata mkondo fulani. Chama hicho kimejivuta kutia mkataba wa ushirikiano na Jubilee na hii inaweza kuwa moja ya sababu,” alisema Bw Okumu.

Vyama vya Kanu, Wiper na CCM vilikubali kushirikiana na Jubilee ndani na nje ya bunge. Japo ODM kimekuwa kikiunga serikali bungeni, hakina mkataba kama huo.

Bw Kimunya alisema baadhi ya wabunge walihisi kwamba wangebadilisha orodha ya wanachama kwa sababu ni wandani wa Rais na Bw Odinga.

Akimuunga mkono, Bw Murathe alisema ODM haiwezi kupatia Jubilee matakwa.

“Shughuli hiyo imefungwa. Tuliwafanyia hisani na hawafai kutupatia masharti,” alisema.

Wakati huo huo Wakenya wanasema hatua ya kumtumia mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi kumwakilisha katika kuapishwa kwa rais mpya wa Malawi Lazarus Chakwera’ ni mwanzo wa kumuandaa kuwa mrithi wake.