HabariSiasa

Ndoa ya unafiki

January 13th, 2020 2 min read

Na MWANDISHI WETU

SASA ni wazi kuwa ndoa ya kisiasa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto imesambaratika.

Hii ni licha ya wawili hawa kuendelea kuwapumbaza Wakenya kuwa wangali pamoja katika upeo wa uongozi wa nchi.

Maneno yao hayalingani na vitendo vyao vinavyoonyesha uhusiano ambao kila mmoja anahujumu mwenzake.

Ingawa hawashambuliani moja kwa moja, washirika wa Rais Kenyatta na Dkt Ruto ndio wamekuwa tarumbeta za kutangaza hisia na misimamo yao kwa umma.

Rais Kenyatta pia amekuwa akitoa matamshi kwa mafumbo akimshambulia Dkt Ruto kuhusu masuala tofauti.

Kwa upande wake Dkt Ruto anashikilia kuwa uhusiano wao uko imara na kuwa wanafanya kazi pamoja.

Wandani wa rais wakiongozwa na David Murathe na kundi la ‘Kieleweke’ likiongozwa na wabunge Maina Kamanda (kuteuliwa) na Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini) wamekuwa ndio mijeledi ya kumgonga Naibu Rais.

Kwa upande mwingine, Dkt Ruto naye anatumia kundi la ‘Tangatanga’ likishirikisha baadhi ya wabunge wa Mlima Kenya na Rift Valley kumshambulia Rais Kenyatta.

Hisia kali za wabunge Alice Wahome (Kandara), Moses Kuria (Gatundu Kusini) na Oscar Sudi (Kapseret) ndizo zimekuwa za juu zaidi katika malumbano kati ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto.

Baadhi ya vitendo vya Rais Kenyatta pia zinaonyesha hamdhamini tena mshirika wake hasa katika uwakilishi wake kwenye hafla.

Kulingana na utaratibu, naibu rais ndiye anayefaa kumwakilisha rais kwenye hafla, lakini katika siku za majuzi amekuwa akiwatuma maafisa wa serikali ama wabunge kumwakilisha licha ya Dkt Ruto kuwepo kwenye hafla hizo.

Wiki iliyopita kulitokea mtafaruku katika mazishi ya mamake Mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua wakati Mbunge wa Kieni, Kanini Kega aliposema ametumwa na rais kupatia familia hiyo Sh500,000 za kuifariji licha ya kuwa Dkt Ruto alikuwepo.

Mwaka jana Waziri wa Utumishi wa Umma, Margaret Kobia alimwakilishi rais kwenye hafla iliyohudhuriwa na naibu rais katika Kaunti ya Nyeri.

Vitendo vya maafisa wakuu serikalini wakiongozwa na Waziri wa Usalama, Fred Matiang’i na katibu wake Karanja Kibicho pia zinaonyesha mfarakano unaokumba ndoa ya Uhuruto.

Rais alimdhalalisha Dkt Ruto mwaka jana alipomwondoa kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Mawaziri kuhusu Maendeleo na kukabidhi wadhifa huo kwa Dkt Matiang’i.

Kudhalalishwa kwa Dkt Ruto kupitia maafisa wa serikali nako kumefika upeo mpya ikifichuka kuwa wiki iliyopita alikatazwa kulala katika makao rasmi ya Naibu Rais jijini Mombasa kwa agizo la afisa wa ngazi ya juu serikalini.

Maafisa wa usalama, utawala wa mikoa na mashirika ya serikali pia wamekuwa wakikwepa hafla za naibu rais kwa kile kimejitokeza kuwa ni kuogopa kuadhibiwa kwa kujihusisha naye.

Vita katika ndoa ya wawili hao vimekuwa vikitokota tangu handisheki kati ya Rais na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga mnamo 2018.

Matokeo ya fujo katika urais yamekuwa ni migawanyiko zaidi nchini kwa misingi ya kikabilia na kisiasa, kutatizika kwa mipango ya maendeleo na ongezeko la gharama ya maisha kwa wawili hao kukosa kumakinika katika kutatua matatizo ya wananchi.

Vita vya wawili hao pia vimegawanya chama cha Jubilee huku rais akionekana kutokuwa makini kuhusu kukihusu.

Wakati wa uzinduzi wa ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) mnamo Novemba, Rais Kenyatta alionekana akiangua kicheko wakati Mbunge wa Suna Mashariki (ODM), Junet Mohamed aliposuta Jubilee kwa migawanyiko inayokikumba.

Pia wakati wa uchaguzi mdogo wa Kibra mwezi Novemba Rais hakushiriki kwenye kampeni za Jubilee na baadaye alikejeli wanasiasa wa Jubilee waliovamiwa na makundi ya vijana wa ODM wakati wa shughuli hiyo.