Kimataifa

Ndoa za matineja huigharimu Afrika matrilioni – Benki ya Dunia

November 28th, 2018 1 min read

MASHIRIKA na PETER MBURU

NDOA za matineja huligharimu bara la Afrika angalau Sh6.3 trilioni, Benki ya Dunia imesema.

Ripoti ya benki hiyo kuhusu utafiti huo ilichapishwa katika baraza la Umoja wa Afrika (AU) kuhusu kumalizwa kwa ndoa hizo, katika kongamano lililoandaliwa nchini Ghana wiki iliyopita.

Benki hiyo ilisema kuwa wanapoingia katika ndoa wakiwa na umri mdogo, uwezekano mkubwa ni kuwa wasichana wataacha masomo na mwishowe kupata pesa chache maishani.

Ripoti hiyo ilisema kuwa kwa wastani, wanawake walio na elimu ya shule za upili wana uwezekano mkubwa wa kufanya kazi na kupata mshahara zaidi ya mara mbili, ikilinganishwa na wale ambao hawana elimu yoyote.

Takwimu za mataifa 12 ya Afrika ambayo idadi ya watu wanaoishi humo ni nusu ya idadi ya bara zima ilionyesha kuwa kwa namna zinavyoadhiri masomo ya watoto wa kike, ndoa za mapema zinagharimu mataifa hayo Sh6.3 trilioni.

“Masomo ya shule za msingi kwa watoto wa kike hayatoshi kwani wanapata manufaa makubwa zaidi ya elimu wanapomaliza shule za upili. Hata hivyo, mara nyingi ni kuwa wasichana hawaendelei na masomo wanapoolewa mapema,” akasema Quentin Wondon, mtafiti mkuu wa ripoti hiyo.