Habari

'Ndoa za mitara zitasaidia idadi ya Wapwani kuongezeka'

November 6th, 2019 2 min read

Na MOHAMED AHMED

WANAWAKE katika kanda ya Pwani wamehimizwa kukubali uke wenza ili kuwezesha kuongezeka kwa idadi ya watu eneo hilo.

Baraza la Maimamu na Wahubiri Nchini (CIPK) limeeleza kuwa ni kupitia kuongezeka kwa ndoa ndiko kutawezesha kuongezeka kwa kizazi kitakachoongeza idadi ya wakazi wa Pwani.

CIPK imetoa pendekezo hilo kwa wanawake baada ya matokeo ya sensa kama yalivyotolewa Jumatatu kuonyesha kuwa kaunti tatu za Pwani zipo miongoni mwa zile ambazo zina idadi ndogo zaidi ya watu.

Kulingana na takwimu za matokeo hayo, Kaunti ya Lamu ndiyo iliyoongoza kutroka nyuma kwa kuwa na idadi ya watu wachache zaidi humu nchini kwa kuwa na watu 143,920 ikifuatwa na ile ya Isiolo ambayo ina watu 268,002 katika idadi yake.

Kaunti ya Samburu ikatajwa kuwa na watu 310,327, huku ya Taita Taveta ikiwa na watu 340,671 na ile ya Tana River ikiwa na watu 315,943.

Jumanne, katibu mtendaji wa CIPK Sheikh Mohamed Khalifa amesema kuwa kuna haja ya kuhimizwa kuongezwa kwa wakazi wa Pwani kuoana.

“Tukizidisha ndoa ndipo tutapata watoto na kufanya idadi yetu iongezeke hata zaidi. Tumekuwa tukiacha mafunzo ya dini na tamaduni zetu na kufuata mienendo ya Wazungu kwa kuzaa watoto wachache,” amesema Sheikh Khalifa.

Amesema kuwa wanawake wakitoa vizuizi kwa waume zao kuoa mke zaidi ya mmoja na vijana nao watie juhudi za kuoa na kupata watoto, basi idadi ya wakazi wa Pwani itaongezeka pakubwa.

Sheikh Khalifa alizungumza baada ya Taifa Leo kutoa kichwa cha habari katika gazeti lake la Jumatatu lililoeleza kuwa eneo la Pwani huenda likawa limelegea chumbani.

Kichwa hicho cha habari kilizua hisia tofauti nchini hasa kanda ya Pwani huku wakazi wa eneo hilo wakishinikiza wanaume kuacha utumizi wa dawa za kulevya ambazo yumkini zinalemaza katika uzazi.

“Utumizi wa miraa na mugoka umekuwa juu; jambo ambalo huenda pengine limechangia Wapwani kupata watoto wachache na ndio maana idadi yetu ipo chini,” akasema Bw Khamis Omar, mkazi wa Mombasa.