Michezo

Ndondi: Friza Anyango amkung’uta Chiroy Maria wa Guatemala

March 9th, 2024 1 min read

Na CHARLES ONGADI

BONDIA Friza Anyango alimkung’uta Chiroy Maria wa Guatemala katika mashindano ya dunia kufuzu Michezo ya Olimpiki mjini Busto Arzizio nchini Italia, Ijumaa.

Ushindi wa Anyango katika pigano hilo la uzito wa ‘welter’ umeipatia Kenya matumaini makubwa ya kufuzu kushiriki Michezo ya Olimpiki.

Tangu Mashindano ya Dunia yaanze mnamo Machi 3, 2024, mabondia wa Kenya wamekuwa wakijipata pabaya wakilambishwa sakafu katika mapigano yao.

Ushindi wa Anyango ulipongezwa na wadau wengi wa mchezo huo nchini, akiwemo mshindi wa medali ya shaba katika Michezo ya Olimpiki Ibrahim ‘Surf’ Bilali na aliyekuwa naibu kocha wa timu ya taifa ‘Hit Squad’ Hongo Kauma.

Naye Shaffi Bakari alipepetana na Rustamov Umid wa Azerbaijan katika uzani wa unyoya lakini Mkenya huyo akaonyeshwa mlango wa ‘exit’. Matokeo haya yaliacha Kenya na bondia mmoja pekee mashindanoni kati ya sita waliopeperusha bendera ya taifa.

Kenya inawakilishwa na mabondia sita katika mashindano haya ya kwanza ya dunia ya kufuzu kushiriki Olimpiki lakini watano walipoteza makabiliano dhidi ya wapinzani wao.

Aidha, mashindano ya mwisho ya dunia kufuzu kushiriki Olimpiki yameratibiwa kuandaliwa Mei 26 hadi Juni 2, 2024, jijini Bangkok, Thailand ambapo Kenya itakuwa na nafasi nyingine ya kujaribu bahati yake.

Michezo ya Olimpiki ya Paris, Ufaransa inatarajiwa kuanza Julai 23 hadi Agosti 8, 2024.