Michezo

Ndondi: Nahodha wa Kenya apigwa ‘stop’ juhudi za kufuzu Olimpiki

March 7th, 2024 1 min read

Na CHARLES ONGADI

MATUMAINI ya nahodha wa timu ya taifa ya ndondi kufuzu kushiriki Michezo ya Olimpiki itakayoandaliwa jijini Paris, Ufaransa yalisambaratika baada ya kushindwa kwa njia ya ‘knock-out’ nchini Italia mnamo Jumanne.

Mogunde anayezichapa katika uzani wa ‘lightmiddle’ alikomolewa na Knezevic Petar Kresimir wa Croatia katika dakika ya pili, raundi ya pili.

Ilibidi refa wa pigano hilo, Thampu Nelka Shiromala, kuruka kati kumwokoa Mogunde aliyekuwa anapokezwa kipigo kizito na Kresimir aliyegeuka simba marara ulingoni.

Kipigo hicho kilitokea siku moja tu baada ya bondia mwingine wa Kenya Christine Ongare kukomolewa kwa wingi wa alama na Guo Yi Xuan wa Taipei katika pigano la uzani wa ‘fly’.

Bondia mwingine wa Kenya–Elizabeth Andiego (middle)–alipanda ulingoni Jumatano kusaka nafasi ya kufuzu.

Hata hivyo Andiego alilemewa na Sontuke Gabrielle wa Lithuania.

Naye David Karanja (fly) anatarajiwa kuzichapa dhidi ya mshindi kati ya Tam Chun Hin wa HKG na Bibossiv Sanken wa Kazakhstan leo Alhamisi.

Bondia Friza Asiko anayezichapa katika uzani wa ‘welter’ na mwenzake Shaffi Bakari wa uzani wa ‘unyoya’, wameratibiwa kupanda ulingoni Ijumaa.

Kenya inawakilishwa na mabondia sita katika mashindano haya ya kwanza ya dunia ya kufuzu Olimpiki.

Michezo ya Olimpiki za Paris itaanza rasmi Julai 26, 2024, na kukamilika mnamo Agosti 11, 2024.