Michezo

Ndoro ya Arsenal kucheza Europa yatimia

August 2nd, 2020 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

LICHA ya kuambulia nje ya mduara wa sita-bora kwenye kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu, Arsenal watanogesha soka ya Europa League muhula ujao wa 2020-19.

Hii ni baada ya masogora hao wa kocha Mikel Arteta kuwapokeza Chelsea kichapo cha 2-1 katika fainali ya Kombe la FA – mashindano ambayo yamekuwa sehemu muhimu katika historia ya soka ya Uingereza kwa zaidi ya mika 150 iliyopita. Fainali ya mwaka huu ilichezewa ugani Wembley, Uingereza mnamo Jumamosi.

Ushindi kwa Chelsea katika gozi hilo la Agosti 1 ungaliwapa Wolves walioambulia nafasi ya saba kwenye jedwali la EPL msimu huu kwa alama 59 sawa na Tottenham Hotspur, fursa ya kushiriki Europa League muhula ujao.

Zaidi ya kufuzu kwa soka hiyo ya bara Ulaya, Arsenal walijizolea pia kima cha Sh504 kutokana na ushindi wao wa Kombe la FA. Chelsea ambao kwa sasa wanajiandaa kurudiana na Bayern Munich ya Ujerumani kwenye hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), walipokea nusu ya kiasi hicho cha fedha.

Arsenal na Chelsea walijishindia pia Sh252 milioni kila moja kwa kuibuka washindi wa nusu-fainali za Kombe la FA dhidi ya Manchester City na Manchester United mtawalia. Aidha, washindi wanne wa robo-fainali walitia kapuni Sh100 milioni kila mmoja.

Fowadi na nahodha Pierre-Emerick Aubameyang alifunga mabao yote mawili ya Arsenal ambao kwa sasa ni wafalme mara 14 wa Kombe la FA. Nyota huyo mzawa wa Gabon, sasa ndiye Mwafrika wa kwanza kuwahi kunyanyua ubingwa wa taji hilo. Alikuwa pia shujaa na mfungaji wa mabao yote ya Arsenal katika ushindi wa 2-0 uliowawezesha kudengua mabingwa watetezi Man-City kwenye nusu-fainali.

Inasadifu kwamba Arsenal waliwapepeta pia Man-City (2-1) kwenye nusu-fainali ya Kombe la FA mnamo 2016-17 kabla ya kunyanyua ubingwa wa msimu huo kwa kuwacharaza Chelsea 2-1 kwa mara nyingine katika fainali.

Mnamo Jumamosi, Chelsea walichukua uongozi chini ya dakika tano za kipindi cha kwanza kupitia kwa fowadi chipukizi mzawa wa Amerika, Christian Pulisic aliyeondolewa uwanjani mwishoni mwa kipindi cha pili kutokana na jeraha la paja.

Aubameyang aliwafungulia Arsenal ukurasa wa mabao kupitia penalti ya dakika ya 28 baada ya kuchezewa visivyo na beki na nahodha wa Chelsea, Cesar Azpilicueta aliyeshindwa pia kukamilisha mechi kwa sababu ya jeraha. Bao la pili la Arsenal lilifungwa katika dakika ya 67

Mbali na kuyumbishwa na majeraha, Chelsea walikabiliwa pia na pigo la kufurushwa ugani kwa kiungo mzawa wa Croatia, Matteo Kovacic aliyeonyeshwa kadi ya pili ya manjano kwa kosa la kumchezea ngware kiungo Granit Xhaka katika dakika ya 73.

Arteta anakuwa mtu wa kwanza kuwahi kuongoza Arsenal kunyanyua Kombe la FA akiwa nahodha na kocha.

Anakuwa pia kocha wa kwanza kuongoza Arsenal kutia kibindoni taji la haiba kubwa katika msimu wa kwanza wa ukufunzi tangu 1986-87 wakati mikoba ya Arsenal ilikuwa ikidhibitiwa na George Graham.

Chelsea wamepoteza fainali tatu kati ya 10 zilizopita katika Kombe la FA dhidi ya Arsenal ambao wameibuka washindi wa fainali zao zote saba zilizopita za Kombe la FA tangu 2002. Hakuna kikosi kingine cha soka ya Uingereza kinachojivunia ufanisi huo katika kivumbi hicho.

Tangu Februari 2018, Aubameyang amefungia Arsenal jumla ya mabao 70 katika mashindano yote. Kibarua kikubwa kwa sasa kilichopo mbele ya Arsenal ni kushawishi sogora huyo wa zamani wa Borussia Dortmund kurefusha mkataba wake uwanjani Emirates hasa ikizingatiwa kuwa anahemewa pakubwa na Barcelona, Real Madrid, Juventus, Chelsea na Inter Milan.

Bao la Pulisic katika fainali ya Jumamosi lilikuwa la kwanza kuwahi kufungwa na mwanasoka mzawa wa Amerika katika hatua hiyo ya Kombe la FA. Kovacic aliweka historia ya kuwa mwanasoka wa sita kuwahi kuonyeshwa kadi nyekundu katika fainali ya Kombe la FA, wachezaji wawili wa mwisho wakiwa wa Chelsea. Victor Moses wa Chelsea alionyeshwa kadi nyekundu katika fainali ya 2016-17 dhidi ya Arsenal.

Kipa Willy Caballero wa Chelsea aliweka rekodi ya kuwa mwanasoka mkongwe zaidi kuwahi kuwajibishwa katika fainali ya Kombe la FA akiwa na umri wa miaka 38 na siku 308. Callum Hudson-Odoi wa Chelsea (miaka 19 na siku 268) aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kuchezeshwa na Chelsea katika fainali ya Komebe la FA.