Michezo

Ndoto ya Birgen kushindia Kenya medali yatimia

March 4th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MKIMBIAJI Bethwell Birgen ameshindia Kenya medali yake ya kwanza na ya pekee katika Riadha za Dunia za Ukumbini zinazokamilika mjini Birmingham, Uingereza, Jumapili.

Birgen alivuruga mpango wa Ethiopia kufagia medali zote katika mbio za mita 3,000 aliponyakua nishani ya shaba kwa dakika 8:15.70, sekunde 0.06 mbele ya nambari nne Hagos Gebrhiwet.

Waethiopia Yomif Kejelcha (8:14.41) na Selemon Barega (8:15.59) walizoa medali za dhahabu na fedha, mtawalia.

Mwakilishi mwingine wa Kenya katika kitengo hiki, Davis Kiplangat, alimaliza katika nafasi ya saba kutoka orodha ya wakimbiaji 12 kwa dakika 8:18.03. Mzawa wa Kenya, Shadrack Kipchirchir, ambaye ni raia wa Marekani, aliondolewa mashindanoni kwa kuvunja sheria za mashindano.

Wakenya Hellen Obiri (mita 3,000), Beatrice Chepkoech (mita 1,500), Winny Chebet (mita 800 na mita 1,500), Margaret Nyairera (mita 800) na Vincent Kibet (mita 1,500) walimaliza vitengo hivyo vyao mikono mitupu.

Naye Emmanuel Korir hakushiriki mbio za mita 800 baada ya kufingiwa nje na masuala ya stakabadhi za usafiri kutoka Marekani anakoishi.