Ndoto ya MCAs kupata magari yaanza kuzimika

Ndoto ya MCAs kupata magari yaanza kuzimika

Na IBRAHIM ORUKO

MADIWANI watangojea kwa muda mrefu kabla kupata Sh2 milioni za kununua magari ambayo waliahidiwa na Rais Uhuru Kenyatta, baada ya Mdhibiti wa Bajeti kutilia shaka utaratibu kuhusu utekelezaji wa agizo hilo.

Afisi ya Mdhibiti wa Bajeti jana ilisema kuwa tayari ameidhinisha bajeti za mwaka wa fedha wa 2021/2022 za kaunti zote.

Iliongeza kwamba baadhi ya kaunti zilijumuisha katika bajeti zao mikopo ya magari wala si fedha za bwerere za kununua magari.

Mapema mwaka huu Rais Kenyatta aliagiza kila diwani apewe Sh2 milioni watakazotumia kununua magari.

Rais Kenyatta alisalimu amri baada ya madiwani wa eneo la Mlima Kenya kumtaka awape fedha hizo kabla yao kupitisha Mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI).

Tume ya Kudhibiti Mishahara na Marupurupu (SRC) tayari imeidhinisha Sh4.5 bilioni zitumiwe kununulia madiwani na maspika wao magari.

SRC iligeuza Sh4.5 bilioni zilizokuwa za mikopo ya magari kuwa fedha za bwerere au marupurupu ya usafiri kwa madiwani.

Naibu Mdhibiti wa Bajeti, Bw Stephen Masha, Jumapili alisema itakuwa vigumu kutekeleza mapendekezo hayo ya SRC na kuongeza kuwa wamebaini dosari katika utaratibu huo wa utekelezaji.

Afisi ya Mdhibiti wa Bajeti sasa inataka kupewa ushauri kuhusu namna pendekezo hilo, la kutoa fedha za bwerere kwa madiwani, litatekelezwa.

Mdhibiti wa Bajeti anasema kuwa baadhi ya kaunti zinatoa mikopo ya magari kwa madiwani kwa kutumia sheria ambayo hairuhusu kutolewa kwa magari ya bwerere.

“Kuna baadhi ya madiwani na maspika hawajawahi kuchukua mikopo ya magari. Je, hao watapewa fedha taslimu au watashawishiwa kununua magari?” akahoji Bw Masha kupitia barua aliyotia saini kwa niaba ya mkuu wake, Bi Margaret Nyakango.

Ofisi hiyo pia inataka kujua hatua itakayochukuliwa kwa madiwani ambao walichukua mikopo ya magari na tayari wameilipa yote.

“Tunaomba ushauri wako kuhusu namna ya kubadilisha mikopo ya magari kuwa magari ya bwerere kwa kuzingatia masuala hayo,” ikasema barua hiyo.

“Vile vile, tunataka kujua jinsi tutakavyofanya kuhusu riba ya mikopo ya magari ambayo baadhi ya madiwani tayari wamelipa,” ikaongezea.

Kulingana na sheria, kila diwani anastahili kupewa mkopo wa Sh3 milioni wa nyumba na mkopo wa Sh2 milioni wa gari, kwa kuzingatia na agizo la rais lililotolewa mnamo 2014.

Aliyekuwa Seneta wa Mandera Billow Kerrow anasema ni vigumu kubadilisha fedha za mikopo ya magari kuwa magari ya bwerere bila sheria mahususi kupitishwa na Bunge.

“Haiwezekani kubadilisha mkopo wa gari kuwa fedha zisizorejeshwa, kwa kutoa agizo bila kuidhinishwa na Bunge,” aeleza.

Mdhibiti wa Bajeti jana alisema kuwa yuko tayari kuidhinisha fedha hizo za magari ya bwerere kwa madiwani endapo SRC itatoa ufafanuzi.

You can share this post!

Gachie Soccer yasaka kushiriki soka ya Taifa Daraja la Pili

Kingi akosoa wanaong’ang’ania kusalia ODM