Michezo

Ndoto za Mbappe kuzolea PSG taji la Uefa zazimwa

May 8th, 2024 2 min read

JOHN ASHIHUNDU Na MASHIRIKA

MATUMAINI ya Kylian Mbappe kutwaa ubingwa wa Klabu Bingwa Ulaya akichezea klabu ya Paris Saint Germain (PSG) yaliyeyuka Jumanne usiku baada ya timu hiyo kubanduliwa na Borussia Dortmund ya Ujerumani katika nusu fainali ya michuano hiyo, ugani Parc des Princes.

Pambano hilo la mkondo wa pili limekuwa la mwisho kwa staa huyo wa zamani wa Monaco kuchezea vigogo hao wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) tangu ajiunge nao mwaka 2017 akiwa na umri wa miaka 18.

Mbappe amepanga kuagana na PSG msimu huu wa uhamisho wa kipindi cha joto baada ya kuitumikia kwa misimu saba, lakini ndoto yake ya kucheza kwenye fainali ya Uefa ugani Wembley mnamo Juni Mosi imezimwa Dortmund ambao waliibuka na ushindi wa jumla wa 2-0.

Ili kutimiza ndoto yake, PSG walihitaji kushinda Borussia Dortmund kwa 2-0, baada ya vigogo hao wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kushinda mkondo wa kwanza kwa 1-0 nchini Ujerumani.

Katika mechi ya marudiano ugani Parc De Prince, mshambuliaji huyo wa timu ya taifa ya Ufaransa anayeshikilia rekodi ya mfungaji bora wa muda wote wa klabu hiyo, alijitahidi kubadilisha matokeo hayo ya awali, lakini bao la mlinzi Mats Hummels alilofunga dakika ya 50 lilizima ndoto yake.

Mbappe akisaidiwa na Ousmane Dembele pamoja na Ashraf Hakimi walikuwa miongoni mwa wachezaji bora waliojaribu bila mafanikio kusaidia PSG ipate ushindi katika mechi hiyo ngumu iliyoshuhudiwa na mashabiki wengi, huku PSG wakiachilia makombora 30, manne yakipiga mlingoti wa goli.

Alipohojiwa kabla ya mechi hiyo, Mbappe alikuwa na imani kubwa kuwa PSG walikuwa katika kiwango kizuri cha kupindua matokeo hayo na kuibuka na kusonga mbele.

Katika mechi hiyo muhimu, kocha Luis Enrique alipanga kikosi chake bila beki mahiri, Lucas Hernandez aliyepata jeraha hapo awali ambalo litamweka nje hadi msimu ujao.

Kocha wa Dormund, Edin Terzic aliwapongeza wachezaji kwa ushindi huo, huku akiwataka wakamilishe safari kwa kutwaa ubingwa mnamo Juni 1.

“Kikosi kimeshirikiana vizuri tangu tucheze na PSV Eindhoven katika raundi ya 16-bora. Wengi hawakuamini niliposema safari ya kwenda London ni fupi. Itawachukuwa siku kadhaa ili waamini niliyosema. Tayari furaha ni tele. Tumeimarika bila ya kila mechi na matunda ndio haya. Tulikuwa makini zaidi dhidi ya PSG, tukifahamu umuhimu wa mechi yenyewe,” aliongeza kocha huyo Mjerumani aliye na umri wa miaka 41.

Dortmund wamefuzu kwa fainali ya Uefa wakati wanakamata nafasi ya tano katika msimamo wa Bundesliga licha ya matokeo ya mchanganyiko.