Habari Mseto

‘Ndovu’ Arsenal juu ya mti avisha Chelsea aibu ya 5-0

April 24th, 2024 1 min read

Na MWANGI MUIRURI

MABAO ya Leandro Trossard (dakika ya 4), mawili ya Ben White (dakika za 52 na 70) na mawili ya Kai Hervetz (dakika za 57 na 65) yalitambisha Arsenal hadi kujithibiti juu ya jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa pointi 77.

Arsenal licha ya kuwa na mzaha mwingi katika kipindi cha kwanza, iliishia kuwika kinyume na matarajio ya wafuasi wa timu za Manchester United, Liverpool na Manchester City.

Mechi hiyo ilichezewa katika uga wa Emirates ambao ndio nyumbani kwa Arsenal.

Ni mechi ambayo Chelsea ilitamalaki kwa kiwango kikuu kwa kuwa ilimiliki mpira guuni kwa asilimia 56 dhidi ya 44 ya Arsenal na ikatandaza pasi 630 dhidi ya 497 za washindi.

Arsenal ilipiga mashuti 27 ya kusaka mabao kati yayo 10 yakilenga michuma huku Chelsea ikifanikiwa fataki saba pekee na ni moja tu ililenga michuma ya Arsenal.

Timu zote mbili zilijipa uhakika wa pasi wa kiwango cha asilimia 88, Arsenal ikicheza ngware mara 12 dhidi ya 11 za Chelsea, kila timu ikijipa kadi mbili za manjano, Arsenal ikichanja kona nne dhidi ya mbili.

Ufanisi huo wa Arsenal sasa umeiacha ikiwa na ujumla wa magoli 56, Liverpool iliyo ya pili kwa jedwali ikiwa na 43 nayo Man City iliyo ya tatu ikiwa na 44.

Liverpool itavaana na Everton leo Jumatano usiku huku Man City ikijirusha ugani Alhamisi usiku dhidi ya Brighton na Jumapili ivaane na Nottingham Forest ndipo iafikie mechi 34 kama Arsenal.

Iwapo Man City itashinda mechi hizo mbili, basi itaipiku Arsenal juu ya Jedwali kwa ujumla wa pointi 79 nayo Liverpool ikishinda leo usiku iwe ya pili kwa pointi 77 lakini idunishwe na Arsenal kwa ubora wa mabao.

Arsenal kwa sasa pia ndiyo imetoka ugani mara nyingi zaidi (15) kwa kutofungwa bao lolote ikifuatwa na Everton (10)m Newcastle (10) na Fulham ambayo imeponyoka kutikisiwa nyavu mara tisa.

[email protected]