Ndugu waliouawa na polisi wazikwa wengine wanne wakiuawa Kajiado

Ndugu waliouawa na polisi wazikwa wengine wanne wakiuawa Kajiado

GEORGE MUNENE na WINNIE ONYANDO

WABUNGE sita kutoka eneo la Mlima Kenya wameshutumu serikali kwa kutowachukulia hatua waliowaua ndugu wawili katika mji wa Kianjokoma, Kaunti ya Embu.

Wakiwa kwenye mazishi ya ndugu hao wawili, wabunge hao walisema Emmanuel Mutura, 19 na Benson Njiru, 22 waliuawa na polisi na serikali imeshindwa kuwakamata waliohusika.

Wabunge Moses Kuria ( Gatundu South), Eric Muchangi ( Runyenjes), John Muchiri (Manyatta), Rigathi Gachagua ( Mathira), Muriuki Njagagua (Mbeere Kaskazini) na Cecily Mbarire (maalumu) walisema wamechoshwa na serikali ya Rais na hata kumtaka Waziri wa Usalama kujiuzulu.

“Tunataka Dkt Fred Matiangi ajiuzulu ikiwa ameshindwa kuwatia nguvuni wahalifu waliowauwa ndugu hawa wawili,” akasema Bw Kuria.

Walipatia serikali siku saba ili kuwasaka na kuwatia nguvuni waliofanya tendo hilo la unyama.

“Ikiwa polisi waliowaua ndugu hawa wawili hawatatiwa nguvuni, tutaandamana na wananchi. Tuko tayari kufa ili haki itendeke,” akasema Bi Mbarire.

Kadhalika, walitaka mageuzi ya haraka katika huduma ya polisi kaunti hiyo huku wakisema polisi waliopo hawajali maslahi ya wananchi.

Kwa upande wao, Spika wa Bunge, Justin Muturi na naibu gavana wa Embu, David Kariuki waliwashutumu polisi kwa kujaribu kuwatetea na kuwalinda polisi waliotenda uhalifu huo.

Naye kinara wa Chama cha Mawakili nchini, Nelson Havi aliwaunga mkono wabunge hao akisema kuwa ndugu hao waliuawa na polisi.

“Ikiwa wahalifu hawatachukuliwa hatua, mimi na mawakili 2,000 tutaandamana hadi haki itendeke,” akatishia Bw Havi.

Haya yanajiri huku visa vya vijana kuuawa katika hali ya kutatanisha vikiendelea.

Mnamo Jumapili, ndugu wawili na binamu zao wawili waliuawa kwa kushukiwa kuwa wezi wa mifugo eneo la Kitengela, Kaunti ya Kajiado.

Vijana walikuwa wameenda kununua kuku kusherehekea siku ya kuzaliwa ya mmoja wao walipokumbana na mauti. Waliouawa ni Fred Mureithi, 30, kaka yake Victor Mwangi aliyekuwa akiadhimisha miaka 25 na binamu zao Mike George, 29 na Nicholas Musa, 28.

Ilisemekana miongoni mwa waliowashambulia ni wanachama wa Nyumba Kumi.

Kamanda wa polisi Kaunti ya Kajiado Muthuri Mwongera alisema wanne hao waliuawa Agosti 8 jioni kwa kushukiwa kuwa wezi wa mifugo.

You can share this post!

Raila asema amepata mbinu kuteka Mlima

Hospitali yakiri kulemewa na wagonjwa wa corona