Habari Mseto

Ndugu wawili ndani kwa kuua mpenzi wa mama yao

June 5th, 2019 1 min read

PIUS MAUNDU na GEORGE ODIWUOR

MAAFISA wa upelelezi jana waliwahoji ndugu wawili wanaodaiwa kumuua mpenzi wa mama yao katika kijiji cha Kyale, Kaunti ya Makueni.

Boniface Masavu, 30, na Kyalo Masavu, 25, walikamatwa Jumanne na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Kilome ili kuhojiwa kuhusiana na mauaji ya Kiendi Kivuva, 52.

Mama yao, Angelica Masavu, 50, pia alikamatwa ili kusaidia makachero kubaini kiini cha mauaji hayo yaliyoshtua kijiji kizima.

Marehemu, ambaye kufikia siku yake ya mwisho duniani alikuwa msimamizi wa baa moja katika soko la Kilome, alikuwa mgeni wa mara kwa mara nyumbani kwa Bi Masavu licha ya uhasama aliopokea kutoka kwa watoto watano wa mama huyo.

Duru zilizomfahamu kwa karibu ziliambia Taifa Leo kuwa Kivuva alikuwa akipitia kipindi kigumu wakati huo baada ya ndoa yake kuvunjika.

“Ingawa marehemu na mama huyo hawakuwa wakiishi pamoja, uhusiano wao ulikuwa wazi,” Kaimu Naibu Kamishna wa Kaunti, Bi Rabecca Ndirangu, alisema kwenye mahojiano.

Polisi walisema ndugu hao wawili walimshambulia mwanamume huyo kwa panga na vifaa butu alipoenda kumtafuta mama yao Jumatatu usiku.

Jumanne alfajiri, jamaa mmoja wa Bi Masavu pamoja na jirani aliyesikia kelele za usiku uliopita, walipata na mwili wa Kivuva ukiwa umetupwa ndani ya mtaro mita 300 kutoka eneo la shambulio.

Kwingineko, mwanamke mwenye umri wa miaka 62 aliuawa Jumanne jioni katika kata ndogo ya Kasewe B, kaunti ndogo ya Rachuonyo Mashariki, Kaunti ya Homa Bay kwa madai ya kuwa mchawi.

Mary Achieng’ aliuawa na kundi la waendeshaji bodaboda waliomshutumu kwa kumuua mvulana wake miezi mitatu iliyopita.

Wahudumu hao kutoka kituo cha kibiashara cha Misambi, walimshambulia mama huyo alipokosa kufichua mganga ambaye alisema walishirikiana kumuangamiza mvulana wake.

Wanakijiji walidai Bi Achieng’ amekuwa akisumbuliwa na mapepo yamarehemu, hususan akiwa amelala ambapo hupata ndoto mbaya.