Habari Mseto

Nduguye Mildred Odira adai kutishiwa maisha

February 6th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

Ndugu ya marehemu Mildred Odira, ambaye mwili wake ulipatikana mochari wiki moja ya baada ya kutoweka sasa anadai maisha yake yamo hatarini.

Bw Carrington Odira, anasema alifuatwa na watu wawili waliokuwa na pikipiki hadi nyumbani kwake mnamo Jumatatu usiku ambao walikesha nje ya lango wakisubiri kumwarifu kwamba angeuawa asipoacha kufuatilia kesi ya mauaji ya dada yake.

“Watu wawili walitufuata mimi na binamu yangu Bonface Kaseo usiku saa mbili. Leo asubuhi mwendo wa saa moja, nilifungua lango na nikawapata wanaume wawili wakiwa kwenye pikipiki na wakaniambia niachane na kesi ya Mildred au nimfuate dada yangu,” alisema Carrington.

Alisema alipiga ripoti kuhusu vitisho hivyo katika kituo cha polisi cha Tassia. Hata hivyo, alisema hatatishwa aache kufuata kesi ya mauaji ya dada yake.

“Hata wakiendelea kutoa vitisho, sitaogopa, ikiwa kesi ya Milly itanifanya nife, niko tayari, na iwe hivyo,” alisema.

“Ni jambo lenye uchungu mtu kumchinja mtoto wenu kama Mildred kisha aje kukutisha. Wacha waje na kuniua lakini ukweli lazima utajitokeza,” alisema.

Mnamo Jumatatu, mbunge wa Mbita Millie Odhiambo aliwataka polisi kufanya uchunguzi kwa upana akisema huenda mauaji ya Bi Odira yalipangwa au hayakuwa yamepangwa.

“Tuliwaambia polisi wafanye uchunguzi kwa upana. Huenda kuna watu waliokuwa wamepanga kumuua lakini pia kuna uwezekano ulikuwa uhalifu ambao haukupangwa lakini hata katika uhalifu usiopangwa, wahusika wanaweza kufanya juu chini kuficha vitendo vyao ikiwa ni pamoja na kutoa vitisho,” alisema Bi Odhiambo ambaye ni wakili.

Mwili wa Bi Odira, aliyekuwa mfanyakazi wa kampuni ya Foresight akihudumu katika Nation Media Group, ulipatikana Jumatatu asubuhi katika mochari ya jiji la Nairobi ukiwa na majeraha mabaya.

Ndugu yake alisema ulikuwa na majeraha usoni, shingoni na tumboni ambayo yalisababishwa na kifaa chenye makali.

Miguu yake ilikuwa imevunjika ishara kwamba alikuwa amekanyagwa na gari na kulikuwa na uwezekano alikuwa amebakwa.

Bi Odira alitoweka Jumanne wiki jana alipokodisha teksi kumpeleka hospitali baada ya kuugua usiku. Polisi wanamzuilia mwenye teksi hiyo huku uchunguzi ukiendelea.