NEMA: Walionyakua ardhi ufuoni na sehemu ya bahari waonywa Lamu

NEMA: Walionyakua ardhi ufuoni na sehemu ya bahari waonywa Lamu

Na KALUME KAZUNGU

WANAOENDELEZA ujenzi wa majumba na miradi mingine kwenye ardhi za ufuo, Kaunti ya Lamu wameamriwa kukoma na kuhama mara moja.

Kumeshuhudiwa ongezeko la wavamizi wa ardhi za ufuo kwenye sehemu mbalimbali za Lamu katika siku za hivi karibuni.

Wanyakuzi hao wameshuhudiwa wakijenga majumba karibu na bahari ilhali wengine wakizingira ua ardhi zilizoko ufuoni na hata ndani ya bahari Hindi.

Miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa zaidi na uvamizi huo ni Wiyoni, Mtangawanda, Pate, Faza, Kizingitini, Ndau, Kiwayu, Kiunga, Matondoni, Kwasasi, Mokowe na Kizuke.

Hali hiyo imeisukuma Mamlaka ya Uhifadhi wa Mazingira nchini (NEMA) kujitokeza na kutoa onyo kali kwa wanaoendeleza miradi husika kuisitisha na kuhama la sivyo waandamwe kisheria.

Mkurugenzi wa NEMA, Kaunti ya Lamu, James Kamula, alisema tabia ya wakazi kuvamia ardhi za ufuoni ilianza tangu jadi hata kabla ya sheria inayodhibiti sehemu hizo kubuniwa nchini.

Bw Kamula aidha alisema NEMA tayari imeanza kutekeleza sheria hiyo na akaahidi kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayepatikana akikaidi sheria hiyo.

Alisisitiza kuwa ardhi zote za ufuoni zilizoko ndani ya umbali wa mita 60 kutoka baharini ni za umma na kwamba yeyote anayeendeleza miradi ya kibinafsi kwenye sehemu hizo anakiuka sheria.

“Sheria imeweka wazi kwamba ni marufuku kwa yeyote kujenga nyumba au kuendeleza mradi wa kibinafsi kwenye sehemu zilizoko ndani ya mita 60 kutoka baharini. Sehemu hizo ni za umma na lazima ziheshimiwe,” akasema Bw Kamula.

Tangazo la NEMA kuhusu ardhi hizo za ufuoni limepokelewa vyema na wazee na wavuvi wa Lamu ambao kwa miaka mingi wamekuwa mstari wa mbele katika kupigania ardhi hizo zisitwaliwe na wawekezaji wa kibinafsi.

Diwani wa zamani wa Lamu, Kassim Omar alisema ni jambo la kusikitisha kwamba wananchi na hata viongozi wamekuwa wakiendeleza miradi yao kiholela kwenye sehemu hizo za ufuoni bila mwelekeo.

“Ukienda Wiyoni, Mtangawanda na Pate, utajionea majumba yakijengwa karibu na bahari. Wengine hata wamezingira sengengendani ya maji baharini. Hili ni jambo lisilofaa. Nafurahi kwamba NEMA imegundua tatizo hilo na iko tayari kulikabili,” akasema Bw Omar.

Eneo la Mtangawanda. Picha/ Kalume Kazungu

Swaleh Bakari ambaye ni msemaji wa wavuvi, Kaunti ya Lamu alisema wavuvi wamekuwa wakipata matatizo kwa kukosa sehemu za kujipumzisha na kuweka shehena zao za samaki kila wanapotoka baharini.

“Sehemu nyingi ambazo tangu jadi zimekuwa zikitumiwa na sisi wavuvi kupumzika na hata kuhifadhi mizigo yetu tayari zimenyakuliwa na mabwenyenye. Nashukuru kwamba NEMA imeamka kuzuia tatizo hilo,” akasema Bw Bakari.

Juma lililopita, serikali ya kaunti ya Lamu ilitangaza mpango wa kuzikomboa sehemu hizo za wavuvi baharini na kuhakikisha zinapata hatimiliki ili kuzihifadhi kutokana na wanyakuzi.

You can share this post!

Urithi wa Raila wagawa ODM

Kenya, Tanzania zalegeza masharti kuimarisha ushirikiano wa...