Habari Mseto

Nema yafunga kiwanda cha karatasi za nailoni Juja

September 19th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

MAMLAKA ya Kuhifadhi Mazingira (Nema) imefunga kiwanda kimoja cha kutegeneza karatasi za nailoni eneo la Theta, kaunti ndogo ya Juja.

Naibu Mkurugenzi wa Nema katika Kaunti ya Kiambu Bw Daniel Nyamora alisema kufuatia habari za wapelelezi wa polisi walifanikiwa kufikia kiwanda hicho kilichoko katika makazi ya watu.

“Baada ya kuingia ndani ya kiwanda hicho, tulipata mitambo na mashine za hali ya juu na zenye thamani ya Sh5 milioni, zinazotumiwa kutengeneza karatasi hizo. Ni kazi ambayo imeendelea kwa muda wa miezi sita hivi,” alisema Bw Nyamora.

Naibu Mkurugenzi wa Nema, Kaunti ya Kiambu, Bw Daniel Nyamora, akagua karatasi za nailoni zilizotengenezwa kwenye kiwanda kimoja eneo la Juja. Picha/ Lawrence Ongaro

Alisema tayari wafanyakazi wawili waliokuwa kwenye kiwanda hicho wakiendesha shughuli za utengenezaji karatasi wamekamatwa na kupelekwa kituo cha polisi cha Juja huku wakitarajiwa kufikishwa mahakamani.

“Uchunguzi wetu unaonyesha kuwa karatasi hizo mara baada ya kutengenezwa kiwandani hapa huuzwa maeneo ya Githurai, Ruiru, na hata Nairobi,” alifafanua mkurugenzi huyo.

Afisa mkuu wa Nema eneo la Thika Bi Charity Wa Kaara aliwaonya wananchi wawe macho wasije wakaingilia biashara hiyo ya kuuza karatasi hizo.

“Yeyote atakayenaswa na karatasi hizo atajipata pabaya kwa sababu atatozwa faini kubwa,” alisema Bi Kaara.

Uchafuzi mazingira

Alisema pia ni hatia kwa mshukiwa huyo kuendesha biashara hiyo kwenye makazi ya watu kwa sababu ya kuharibu mazingira na kusababisha makelele akitumia mitambo yake.

“Ninawahimiza wananchi popote walipo kushirikiana na afisi yake ili kusaidia maafisa wake kutekeleza wajibu wao kwa urahisi,” alisema afisa huyo.

Afisa mwingine wa mazingira eneo la Kiambu, Bw George Mwangi Muchue, alisema watu wengi bado wanaendelea kutumia karatasi hizo kufungia na kupakia sukumawiki, miraa, na hata sukari.

“Tunapata changamoto tele tunapoendesha msako wetu kwa sababu maeneo mengine wananchi huzua fujo jambo linaloponza juhudi zetu kutekeleza wajibu wetu ipasavyo,” alisema Bw Muchue.

Alisema karatasi hizo kusambazwa kwenye maduka usiku wa manane.

“Kwa hivyo tungetaka tupewe ulinzi wa kutosha ili kukabiliana na changamoto yoyote itakayofika mbele yetu,” alisema afisa huyo.

Bw Humphrey Etemesi ambaye pia ni afisa wa mazingira alitaja maeneo kunakoendeshwa biashara ya karatasi hizo kwa wingi kama Githurai, Kimandura, na Ruiru.

Alisema biashara hiyo huendeshwa usiku kwa sababu wanaoizamia wanahisi hakuna anayeweza kuwapata wakati kama huo.

“Hata hivyo, tutatafuta mikakati jinsi ya kuwanasa watu hao usiku ili tuangamize biashara hiyo kabisa,” alisema Bw Etemesi.