Habari Mseto

NEMA yapendekeza 'tuktuk bubu' kupunguzia Wakenya kelele mijini

June 28th, 2019 1 min read

Na DIANA MUTHEU

JINA tuktuk huwa linatokana na sauti inayotolewa na magari hayo, lakini sasa tuktuk zisizo na kelele zimeanza kuuzwa nchini.

Mkuu wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Uhifadhi wa Mazingira (NEMA) tawi la Mombasa, Bw Stephen Wambua alisema aina hiyo mpya ya tuktuk inafaa sana nchini kwa kuwa zitapunguza kelele jijini hasa katika miji inayotegemea zaidi magari hayo kwa uchukuzi wa umma kama vile mji wa kitalii wa Mombasa.

“Hii ni hatua nzuri kwa kuwa barabarani na hata vitongojini kelele itapungua,” Bw Wambua alisema.

Aliongeza kuwa njia mpya ya kupunguza uchafuzi wa hewa na moshi utokao kwa tuktuk hizi pia inapaswa kubuniwa.

“Ikiwa hii inaweza kuunganishwa na teknolojia za kupunguza uchafuzi wa hewa na moshi, basi mazingira yetu yatahifadhiwa. Kwa pamoja, kelele nyingi na uchafuzi wa hewa utapungua,” Bw Wambua aliongeza.

Kwa muda mrefu tuktuk zimeonekana kuwa chanzo cha kelele mingi mijini na hata kuzua mzozo kati yao na serikali ya kaunti ya Mombasa ambayo iliwaamuru kutoingia katikati mwa mji, suala lililowaghadhabisha wawekezaji katika sekta hiyo.

Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa tuktuk hizo ziitwazo TVS Duramax, Bw Bahaj Nassir ambaye ndiye mkuu wa mauzo ya tuktuk katika kampuni ya Abson Motors, Mombasa alisema kuwa miundo hiyo itasaidia kupunguza kelele na kufanya usafiri katika sekta hii kuwa wa kuvutia.

“Kelele itapungua na abiria watasafiri kwa amani,” Bw Nassir alisema.

Tuktuk hizi pia zina spika mbili za redio, unaweza kutumia USB kuweka moto kwa simu na pia ina maji ya kupooza injini inapokuwa moto sana. Tuktuk hizi mpya zinauzwa Sh375, 000.

Mwenyekiti wa chama cha wamiliki na madereva wa tuktuk (TODA), Bw Obedi Muruli alisema mabadiliko hayo yatabadili sekta hiyo na kuifanya ivutie zaidi kwa kuwa yanahifadhi mazingira.

“Haya ni baadhi ya mabadiliko mazuri ambayo kama sekta tunapaswa kuyafanya kila wakati,” Bw Muruli alisema.