Habari Mseto

Nema yawaonya wanaomiliki maeneo ya uchimbaji mawe bila leseni

October 19th, 2020 2 min read

Na MISHI GONGO

MAMLAKA ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) imeowaonya wakazi wa Kwale wanaomiliki maeneo ya uchimbaji mawe bila leseni.

Walisema sehemu hizo zinazohudumu kinyume na sheria ni hatari kwa maisha ya wanaofanya kazi katika sehemu hizo kutokana na kuwa hali ya usalama haijatathminiwa na kukubalika kuwa salama kwa shughuli ya uchimbaji mawe.

Wiki iliyopita watu wawili walipoteza maisha yao baada ya kufunikwa walipokuwa wakichimba mawe katika eneo la Maweni eneobunge la Msambweni.

Hali hiyo iliifanya mamlaka hiyo kufunga sehemu ya mkasa ili kufanya utathmini.

Mkurugenzi wa NEMA katika kaunti hiyo Bw Godfrey Wafula alisema kuwa ndani ya miezi mitatu, wamepoteza watu watatu katika mikasa ya kuta za mashimo kuporomoka.

Kufuatia mikasa hiyo mamlaka hiyo iliagiza kufungwa kwa maeneo hayo wakisema kuwa si salama kwa wenyeji.

Wakati huo huo aliwaonya watakaopatikani wakiendeleza shughuli za uchimbaji mawe katika sehemu zilizofungwa akisema kuwa watachukuliwa hatua.

Kulingana na mkurugenzi huyo alieleza kuwa sehemu hiyo itaendelea kufungwa hadi pale usalama wa sehemu hiyo utakapotathminiwa.

“Kuhudumu katika sehemu ya uchimbaji mawe ambayo haina leseni ni kuhatarisha maisha yenu hivyo ninawashauri mhamie kwa sehemu za uchimbaji ambazo zimeruhusiwa kutumika,” akasema mkurugenzi huyo.

Aliongezea kuwa serikali inaendelea kufanya utathmini ili kuboresha sehemu hizo kudhibiti mikasa ya watu kufunikwa kuta zinapoporomoka.

Kufungwa kwa eneo hilo kulizua rabsha miongoni mwa wenyeji ambao waliikashifu serikali kwa kwa kuwapokonya kitega uchumi chao.

Bw Wafula alisema sehemu hizo ni hatari kwa mazingira na maisha ya wenyeji hasa nyakati za mvua ambapo ardhi huwa hafifu na mchanga telezi.

Aidha, alisisitiza kuwa wako makini kuhakikisha kuwa wanalinda mazingira kutokana na aina yoyote ya uharibifu.

“Kabla ya sehemu ya uchimbaji mawe kufunguliwa, lazima mikakati iwekwe kuhakikisha kuwa mazingira yanalindwa; hakuna uchafuzi wa aina yoyote na usalama wa wataka hudumu katika sehemu hizo unazingatiwa,” akasema.

Akiongezea kuwa miongoni mwa mambo wanayoyaangalia ni kuwa na viingilio na sehemu za kutokea, barabara nzuri na mipango ya kuboresha mashimo yaliyoisha mawe kabla watu kuruhusiwa kurudia shughuli katika sehemu hizo.

Pia aliwashauri wenyeji kutafuta njia mbadala za kujipatia riziki bila ya kuhatarisha maisha yao.

Wachimbaji mawe katika eneo hilo waliiomba serikali kuwapa muda zaidi kuondoa vifaa vyao na mawe waliyokuwa wamekata.