Habari

NENDENI SALAMA: Misa ya kuaga wanafunzi 10 yaandaliwa

August 10th, 2018 2 min read

Na BONIFACE MWANIKI

HALI ya majonzi ilitanda katika uwanja wa michezo wa shule ya upili ya St. Joseph’s Seminary, Mwingi Alhamisi wakati wa misa ya kuwaaga watoto 10 wa shule ya msingi ya St Gabriel waliofariki dunia kwenye ajali ya barabarani mapema wiki hii.

Ndugu, jamaa, marafiki na viongozi mbalimbali waliomboleza watoto hao waliofariki ajalini wakitoka kwenye ziara ya kimasomo mjini Mombasa.

Watoto hao walikuwa Bernard Tio (Darasa 8), James Muthui Munyithya (Darasa 8), Andrea Kasyoka Munyithya (Darasa 8), Caleb Baraka Kavandi (Darasa 7), Winnie Mbete Mumo (Darasa 8), Vivian Wakio Wawira (Darasa 8), Stephen Mulyungi Mwangangi (Darasa 8), Kennedy Matei Malonza (Darasa 8), Joy Wambui Waithaka (Darasa 8), na Joy Mutanu Mwangangi (Darasa 8).

Alhamisi, Serikali ilitangaza kwamba, kila familia iliyofiwa na mtoto itapewa Sh100,000 za kugharimia mazishi.

Waziri wa Elimu Bi Amima Mohamed, alisema wizara yake ilipata pigo kubwa baada ya ajali hiyo iliyowaua watoto hao wadogo.

Ibada hiyo ya wafu iliongozwa na Kasisi mkuu wa Dayosisi ya Nyeri Anthony Muheria na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Gavana wa Kitui, Bi Charity Ngilu.

Viongozi wengine walikuwa ni pamoja na Kiongozi wa Chama cha Wiper Stephen Kalonzo Musyoka, Waziri wa maswala ya Nchi za Kigeni Monica Juma, Katibu mkuu katika wizara ya Elimu Dkt Belio Kipsang na wabunge kadhaa wa kaunti ya Kitui.

Akisoma hotuba ya Rais Uhuru Kenyatta, Bi Amina alisema serikali imehuzunishwa na vifo vya watoto hao wadogo.

“Ni huzuni kubwa kuona watoto wenye umri mdogo kama huu wakiangamia kwenye ajali iliyotokana na utepetevu wa binadamu na ambayo ingeweza kuepukwa, iwapo sheria zote zilizowekwa zingeweza kuzingatiwa,” akasema.

Akizifariji familia hizo, Bw Musyoka aliitaka serikali kuu itengeneze barabara ya kutoka Kibwezi kuelekea Kkitui ambayo alisema imechukua miaka mingi.

“Basi hili linasemekana kutumia barabara ya kutoka Kibwezi kuja Kitui, dereva akitarajia kufika mapema kabla ya muda uliowekwa na wizara ya Elimu. Lakini kutokana na ubovu wa barabara hii, haingewezekana,” akasema.

Dkt Kipsang kwa upande wake alizitaka shule zote nchini kuzingatia amri ya rais ya kutaka magari yote ya shule kutosafiri ifikapo saa kumi na mbili jioni.

“Ni vyema kuzingatia amri ya rais ya kuhakikisha kuwa hakuna gari la shule linalosafiri baada ya saa kumi na mbili jioni, hii ni vyema haswa tunapozingatia usalama wa watoto wetu,” alisema Dkt Kipsang.

Pia aliwataka madereva wote wa mabasi ya shule kutafuta malazi kwenye shule zozote za umma au kibinafsi, iwapo saa kumi na mbili jioni itawapata wangali barabarani.

Gavana Ngilu aliwataka viongozi kutoanza kumtilia yeyote lawama kwa kusababisha ajali hiyo, huku akisema serikali yake iko tayari kuwasaidia walioathirika.

Mbunge wa Mwingi ya Kati, Bw Gideon Mulyungi, aliitaka serikali kupitia wizara ya ujenzi kukarabati barabara ya kutoka Thika kuelekea Garissa akisema ni nyembamba mno.’