Lugha, Fasihi na Elimu

NDIVYO SIVYO: Neno ‘hakuna’ lisitumiwe badala ya kikanushi ‘si’

February 21st, 2024 1 min read

SEHEMU YA KWANZA

AGHALABU niliwasikia baadhi ya watu hasa wazee wakitumia neno ‘hapana’ kuwaasa wengine dhidi ya kutenda mambo fulani. Hivi ndivyo walivyosema: ‘Hapana enda kwake’, ‘Hapana sema naye’ na kadhalika.

Leo, matumizi ya neno ‘hakuna’ yamezoeleka miongoni mwa baadhi ya watumizi wa lugha ya Kiswahili kwa maana inayokaribiana sana na ile tuliyoitaja.

Hili la pili hutumiwa vibaya na watu wa umri tofauti yamkini kutokana na sababu mbalimbali.

Kwanza, kutofahamu kanuni za ukanushaji wa vitenzi vya Kiswahili na pili, hiyo huwa njia ya mkato kwao kuwasilisha ujumbe bila kutatizwa na kanuni hizo.

Ijapokuwa ‘hakuna’ ni kitenzi cha Kiswahili katika hali kanushi, hakipaswi kutumiwa kueleza kwamba kitu, hali au jambo fulani halitatendeka. Kikanushi ‘si’, ‘ha’ au ‘hau’ hutumiwa katika mazingira ya pili.

Ni kosa kusema ‘hakuna kulala’ kwa maana ya ‘tusilale’, ‘msilale’ au ‘hatutalala’ – ijapokuwa matumizi ya kwanza hujikita katika mazingira ya kuwahamasisha au kuwachochea watu kutenda mambo kwa njia fulani.

Kitenzi ‘hakuna’ ni ukanushaji wa ‘kuna’. Hiki cha pili ni kitenzi kishirikishi ambacho hutumiwa kuonyesha kuwepo kwa kitu mahali fulani.

Baadhi ya watumizi hupenda kuongezea virejeshi mbalimbali mwishoni mwa kitenzi ‘kuna’ kutegemea ngeli husika ili kukitofautisha na kitenzi kingine chenye maana ya kukwaruza au kukwangua kitu kwa kucha.

Kwa mfano: ‘Kunayo maji kidogo katika ndoo hii’ badala ya ‘Kuna maji kidogo katika ndoo hii’. Katika makala yajayo, nitatoa maoni yangu kuhusu kuongezewa kwa virejeshi tulivyovtaja mwishoni mwa kitenzi ‘kuna’.