Kimataifa

Neno-siri linalotumika zaidi duniani ni 'Liverpool' na '123456' – Utafiti

April 21st, 2019 1 min read

Na Mashirika

MAMILIONI ya watumiaji wa mitandao ya kijamii hutumia neno ‘Liverpool’ au nambari ‘123456’ kama neno lao la siri kote duniani, utafiti umebaini.

Utafiti uliofanywa na Kituo cha Usalama wa Mitandao cha Uingereza (NCSC), ulibaini kuwa mamilioni hutumia nambari ‘123456’ kama nywila na hivyo kutoa mwanya kwa wadukuzi kudukua akaunti zao.

Kituo hicho kilibaini kuwa akaunti milioni 23 zinatumia nambari 123456 kama neno la siri katika mitandao ya Facebook, Twitter, Instagram kati ya mitandao mingineyo ya kijamii.

Utafiti pia ulibaini kuwa idadi kubwa ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wanatumia neno 123456789 au 1111111 kama neno la siri.

Majina ya watu yanayopendelewa kutumika kama neno la siri ni Ashley, Michael, Daniel, Jessica na Charlie.

Majina ya timu za kandanda yanayopendelewa sana ni Liverpool FC na Chelsea.

Kituo hicho kilionya kuwa watu wengi wako katika hatari ya kupoteza fedha au taarifa za kibinafsi mitandaoni kwa kutumia neno la siri ambalo ni rahisi kudukuliwa.