NEOLIN MOMANYI: Hongera NMG kwa kujitolea kuangazia masuala ya wasanii

NEOLIN MOMANYI: Hongera NMG kwa kujitolea kuangazia masuala ya wasanii

Na JOHN KIMWERE

MWANZO wa ngoma kila mja hujipa matumaini ambapo huwa ni hali ya kutarajia. Ni katika kutumainia na kuvumilia ambapo ana imani nyota yake itang’aa na kuibuka mwana maigizo wa kimataifa miaka ijayo.

Neolin Kwamboka Momanyi ambaye kisanaa anafahamika kama Nyabotobe ni mwigizaji pia dansa anayeibukia aliyeanza kujituma katika masuala ya maigizo mwaka uliyopita.

Japo hajapata mashiko, anasema amepania kujibiidisha katika tasnia ya uigizaji anakolenga kufikia kiwango cha msanii wa filamu za Kinigeria (Nollywood), Mercy Johnson. ‘

‘Ndio nimeanza kucheza ngoma lakini nilianza kushiriki maigizo kanisani na shuleni nilipokuwa mdogo,” anasema na kuongeza kuwa ni hatua aliyofikia baada ya kuvutiwa na kipindi cha Papa Shirandula ambacho hupeperushwa kupitia Citizen TV.

Anadokeza kuwa amejikuta katika tasnia ya uigizaji ilhali tangia akiwa mdogo alidhaminia kuhitimu kuwa mwana habari lakini ndoto yake haikutimia kutokana na changamoto za kimaisha. Pia anasisitiza kuwa anatamani sana kushiriki filamu na ifaulu kupeperushwa kupitia stesheni za kimataifa.

Dada huyu alianza kujituma katika masuala ya uigizaji mwaka uliyopita chini ya Egetenga Production akiwa mmoja kati ya wasanii walioshiriki filamu kwa jina Ensio(Jiwe). ”Kando na filamu hiyo nimeshiriki filamu kama ‘Masoja’, na ‘Okiondo Show alipokuwa kama mwanamke wa kijijini ambayo imeonyeshwa kupitia runinga ya mtandaoni iitwayo MoCha TV ambayo humilikiwa na Rose Nyabhate.

Kwa wasanii wa kigeni anasema anatamani sana kufanya kazi na msanii wa Nigeria kama Mercy Johnson aliyeshiriki filamu kama ‘The Poor food Seller,’ na ‘Secret Ties,’ kati ya zingine. Mwingine akiwa, Jacky Appiah msanii wa Ghana anayejivunia kuigiza filamu kama ‘Passion of the Soul,’ na Tangled Affection.”

Anasema ndani ya miaka mitano ijayo amepania kuwa miongoni mwa waigizaji mahiri nchini pia akipokea hela nzuri kutokana na kazi ya maigizo.

”Sio rahisi kuibuka mwigizaji mahiri pia kuchuna hela ndefu katika tasnia hii lakini naomba wenzangu wanaokuja kamwe wasiidharau ni ajira kama nyingine. Tunazidi kushuhudia wana maigizo wengi tu katika mataifa yanayoendelea wakifanya vizuri katika sekta hii,” akasema.

Kipusa huyu anatoa wito kwa Wakenya kuwapa wazalendo sapoti ili kuendelea kukuza tasnia ya filamu nchini na kusaidia waigizaji wanaoibukia. Msanii huyu anashukuru tovuti ya Taifa Leo Dijitali na Gazeti la Mwanaspoti chini ya Shirika la Nation Media Group kwa kuchukua nafasi kuangazia masuala ya waigizaji wa kike nchini.

”Sina shaka kusema kuwa imekuwa vigumu kwa magazeti mengine kuchapisha habari za wasanii chipukizi ambao ndio wanaojijenga kisanaa,” alisema.

Anashauri wenzie wajiamini pia wawe wabunifu ili kuenda sambamba na wakati huu wa ukuaji wa teknolojia. Binti huyu alizaliwa mwaka 1986 katika Kaunti ya Nyamira.

You can share this post!

JOY KINYUA: Serikali ipige jeki uigizaji nchini

Siri ya Young Elephant kutetemesha ligi