Kimataifa

Netanyahu kushtakiwa rasmi kwa ufisadi, asema hatingisiki

November 23rd, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

WAZIRI Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, hatimaye amepatikana na makosa ya ufisadi, na kuwa waziri mkuu wa kwanza wa nchi hiyo kushtakiwa rasmi akiwa mamlakani.

Hata hivyo, Netanyahu alitaja hatua hiyo kama mapinduzi na akasisitiza kuendelea kushikilia usukani.

Tangazo hilo la kushtua liliendeleza utata wa kisiasa unaokumba Isreal ambayo haijakuwa na serikali kwa miezi kadhaa na kuna uwezekano wa kufanyika kwa uchaguzi wa tatu katika kipindi cha mwaka mmoja.

Mwanasheria Mkuu wa Israeli, Avichai Mandelblit aliamua kumshtaki Netanyahu, waziri mkuu aliyehudumu kwa muda mrefu katika nchi hiyo kwa ufisadi, ulaghai na kukiuka kiapo cha afisi yake.

Kwenye hotuba iliyochukua dakika 15, Netanyahu alilaumu mahakama, polisi na idara nyingine kwa kupanga njama kumsingizia madai yaliyochochewa kisiasa.

“Kinachoendelea hapa ni juhudi za kufanya mapinduzi dhidi ya waziri mkuu,” alisema kwenye hotuba iliyopeperushwa kwenye runinga.

“Lengo la uchunguzi lilikuwa ni kunyakua haki kutoka kwa serikali.”

Aliapa kuendelea kuhudumu kama waziri mkuu licha ya kukabiliwa na kesi kortini na shinikizo za kisiasa.

“Nitaendelea kuongoza nchi hii kikamilifu, kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Mpinzani wake mkuu wa kisiasa, Benny Gantz, ambaye amekuwa akijaribu kuunda serikali ya muungano, alisema ilikuwa huzuni kuu kwa Israeli kushtaki kiongozi lakini akamtaka Netanyahu kujiuzulu na kuzingatia mashtaka yanayomkabili.

“Hakuna mapinduzi yoyote Israel, lakini ni wale ambao wamejifungia mamlakani,” alisema.

Netanyahu, 70, ambaye amepachikwa majina ya msimbo “Bw Usalama” na “Mfalme Bibi” amekuwa mamlakani tangu 2009 na ni maarufu mno katika siasa za Israel.

Juhudi kuunda serikali

Kushtakiwa kwake kunajiri kukiwa na juhudi za kuunda serikali baada ya uchaguzi mkuu kufanyika mara mbili na mshindi kukosekana.

Kisheria, Netanyahu hafai kujiuzulu isipokuwa apatikane na hatia baada ya mfumo wa haki kukamilika lakini presha za kisiasa zinatazamiwa kuongezeka.

Anaweza kuomba bunge, inayofahamika kama Knesset, kumkinga asishtakiwe.

Analaumiwa kwa kupokea hongo ya maelfu ya pesa ili kubadilisha kanuni kuruhusu shirika moja la habari kumpendelea katika habari zake.

Mandelblit alisema ilikuwa vigumu na siku ya huzuni kwa Israel kumshtaki kiongozi wake lakini hatua hiyo ilionyesha hakuna raia aliye juu ya sheria.

“Raia wote wa Israel, sisi sote, na hata mimi, tunategemea viongozi waliochaguliwa, na kwanza kabisa akiwa waziri mkuu,” Mandelblit alisema.